Tuesday 26 July 2016

RAIS MAGUFULI KIBOKO, ASHINDA UENYEKITI KWA KUPATA KURA ZOTE ZA WAJUMBE, AMZUIA KINANA KUNG'ATUKA, AAHIDI SERIKALI KUHAMIA DODOMA NDANI YA MIAKA MITANO

RAIS Dk. John Magufuli amechaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa tano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuzoa kura zote zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama, huku akitangaza vipaumbele  vyake katika uongozi wake ndani ya CCM.

Pamoja na vipaumbele hivyo, Dk. Magufuli pia alitangaza na kuomba ridhaa ya wajumbe wa mkutano huo kumkubalia pendekezo lake la kumtaka Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana na Sektetarieti yake kuendelea na nyadhifa hizo mpaka atakapoamua vinginevyo.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kinana kuwasilisha barua aliyoandika jana, akiomba kujiuzulu pamoja na sekretarieti yake ili kumpa nafasi kufanya uteuzi. Kutokana na uamuzi huo wa Dk. Magufuli, wajumbe wa mkutano huo waliridhia kwa kauli moja pendekezo lake.

Dk. Magufuli alichaguliwa jana, kwa kura 2,398 za ndio zilizopigwa na wajumbe hao na kukabidhiwa rasmi uongozi wa Chama na mtangulizi wake, Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete.

Baada ya kutangaza matokeo hayo,  Dk. Kikwete alimkabidhi Rais Magufuli Katiba ya CCM, Kanuni za uongozi na maadili, Kanuni za uchaguzi  katika CCM, Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 na vitabu vingine vya tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Nakukabidhi vitabu vinne vya tathmini ya uchaguzi tuliyoifanya sisi wenyewe inayoonyesha yupi lifanya vipi, tulipata tatizo gani na nani alikuwa tatizo.Ukavisome na kuvifanyia kazi. Baada ya kusema hayo, kazi yangu imekwisha,”alisema  Dk. Kikwete.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa rasmi nafasi hiyo ya mwenyekiti , Dk. Magufuli aliwashukuru wajumbe na kutangaza vipaumbele vyake, ambavyo anatarajia kufanya kwa kushirikiana na viongozi wenzake.

Dk. Magufuli alisema la kwanza anatarajia kuimarisha utendaji kazi ndani ya Chama, kujenga chama chenye uwezo wa kuisimamia serikali na kwamba, viongozi wa Chama ndio watakuwa ‘mabosi’ wa watendaji wote walioko serikalini.

“Uwe makamu wa rais, waziri mkuu, waziri, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya  na hata katibu tarafa, utaongozwa na viongozi wa chama na wana CCM,”alisema na kuongeza kwamba, watendaji watakaoshindwa kujua mabosi wao ni viongozi wa CCM wajiondoe wenyewe.

Eneo lingine ambalo Mwenyekiti huyo mpya wa CCM alisema atalifanyia kazi ni kuangalia muundo wa Chama  na kuhakikisha kinakuwa na safu bora na kuondoa vyeo visivyo na tija kwenye Chama.

Dk. Magufuli alitolea mfano watoto wanaoijiunga na chipukizi, ambao ni kuanzia umri wa miaka 8 hadi 15, kutumika kwenye shughuli za kisiasa badala ya kwenda shule.

Alisema  kuna haja ya suala hilo kuangaliwa upya kwa kuwa kuna hatari kwa vyama vingine kuibuka na makundi ya namna hiyo, badala ya kuwaacha watoto hao kuendelea na mfumo wa elimu.

Mwenyekiti huyo alihoji umuhimu wa uwepo wa makamanda wa vijana , walezi wa jumuia na washauri wa wazazi huku wengi wenye vyeo hivyo wakiwa ni watu wenye fedha.

Pamoja na hilo, alihoji  mtindo wa wanasiasa kujirundikia vyeo huku akitoa mfano  wa waziri kuwa mbunge, kamanda wa vijana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, jambo ambalo alisema linawanyima fursa wanachama wengine kupata nafasi za uongozi.

Aliwataka wanachama wa CCM kuwa mfano kwenye kuongoza mabadiliko ndani ya Chama kwa kuwasimamia watendaji serikalini na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, hatua ambayo itawavutia wananchi kujiunga na chama, kwa kuwa msingi wa chama ni kuwa na idadi kubwa ya wanachama.

Dk. Magufuli alisema katika uongozi wake, atahakikisha anasimamia kanuni na maadili ya uongozi ndani ya Chama na kudhibiti wanachama maslahi na  wala rushwa ambao wamekuwa wakiharibu sifa ya Chama.

“ Chama chetu ni miongoni mwa taasisi ambazo zina tatizo la rushwa. Katika uongozi wangu, kiongozi anayesaka uongozi kwa rushwa, hatakuwa na nafasi.Mimi nitasema ukweli na ukweli utabaki kuwa ukweli,”alisema.

Alisema rushwa imekuwa chanzo cha CCM kupoteza nafasi mbalimbali kutokana na kuteua wagombea wasiokubalika baada ya kutoa fedha na kuwaacha wanaokubalika kwa wananchi wakishindwa kupata nafasi.

Dk. Magufuli alisema katika uongozi, yeyote atakayetoa rushwa hatachaguliwa ndani ya CCM na kurejea uzoefu alioupata wakati wa kinyang`anyiro cha kuwania nafasi ya kuteuliwa na Chama kuwa mgombea urais, ambapo alikumbana na changamoto hizo mkoani Iringa.

“Mimi nachukia rushwa na hata mwenyekiti wetu mstaafu anaichukia. Alituonyesha mfano kwa vitendo kwa kumchinjia mbali rafiki yake (Lowassa) bada ya kugundua ni mtoa rushwa na ni fisadi,”alisema na kuonya kwamba mwakani  kutakuwa na uchaguzi wa Chama, hivyo hatakuwa na simile kwa yeyote atakayetoa rushwa.

Dk. Magufuli alinukuu ahadi  namba tatu ya mwanachama wa CCM, ambayo inasema 'Sitatoa wala kupokea rushwa, rushwa ni adui wa haki'.

USALITI

Mwenyekiti mpya wa CCM ameahidi kupambana na kukomesha usaliti ndani ya Chama huku akisisitiza ni kheri kuwa na mchawi kuliko msaliti kwenye chama. Aliwataka
wanachama wajirekebishe na kutubu kuanzi leo na kama wapo waache au waondoke hata leo.

“Baadhi ya watu ni wasaliti, mchana wako CCM, usiku wanakuwa CHADEMA. Mimi siamini kama wasaliti kama wana CCM wasaliti wanahitajika ndani ya Chama,”alisema.
 
DK. Magufuli alisema pia amedhamiria kuboresha maslahi ya watendaji wa Chama na kuboresha utendaji ndani ya Chama ili uendane na wakati na kwamba atahakikisha chama kinajitegemea kiuchumi.

Alisema kwa kuanzia ataunda kikosi kazi  cha kuhakikisha mali za chama na kutoa wito kwa Katibu Mkuu na watendaji wote wa Chama na jumuia zake  kuorodhesha mali za chama.

Mwenyekiti huyo alisema pia ataboresha mfumo wa ulipaji ada na wanachama wataanza kulipa ada kwa mfumo wa kielektroniki.

Pia alisema atahakikisha wanaongeza idadai ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa CCM na kwamba viongozi waliopita wamefanya kazi kubwa katika kipindi kilichopita kwa kuongeza wanachama kufikia wanachama milioni 8.7.

“Tunahitaji kuongeza wanachama , tuwe na wanachama waaminifu watakaoshiriki katika maendeleo na kuwa na viongozi bora wa mfano wa kuigwa.

Alisema katika miezi nane ya utendaji serikalini amekutana na changamoto nyingi tatizo la upotevu wa mapato na watumishi hewa ambapo serikali yake imefanikiwa kuwaondoa watumishi hewa 12,500.

Dk. Magufuli alisema  na ndani ya CCM kama kuna watumishi hewa nao wataondoka

MAKAO MAKUU KUHAMIA DODOMA

Katika hatua nyingine. Dk.Magufuli aliahidi katika kipindi chake cha miaka mitano atahakikisha makao makuu ya serikali yanahamia Dodoma na kwamba katika hilo hataki kusikia visingizio.

Alisema haoni sababu ya kutohamia Dodoma wakati kuna miundombinu muhimu zikiwemo barabara za lami zinazounganisha  mji wa Dodoma na mikoa mbalimbali.

“Kama Dodoma inaweza kupokea wajumbe wa makutano mkuu, wakakaa wakala na kulala. Vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano vinafanyika Dodoma, sioni sababu ya mimi kuendelea kukaa Dar es Salaam,”alisema na kuongeza baada yay eye kuondoka walio chini yake akiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na watendaji wengine watafuata,”alisema.

Dk. Magufuli aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumuamini kwa mara nyingine na ni katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ateuliwe na CCM kugombea urais.

Alisema ahadi yake ni kwamba hatawaangusha na kwamba katika kipindi cha miezi nane tangu aingie madarakani ameanza kutekelea ahadi  ambazo CCM ilizitoa kwa wananchi wakati wa kampeni.

Dk. Magufuli alitaja baadhi ya ahadi hizo ni ununuzi wa ndege mbili ambazo zitaingia nchini Septemba mwaka huu, ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar, Mwanza,Kigoma na kwamba kwenye bajeti imetengwa zaidi ya sh. trilioni moja.

Alisema pia ameendelea kutekeleza ahadi ya elimu bure kwa kutenga sh. bilioni 18.7 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia elimu, pia serikali ya Tanzania na Uganda imeanza mradi bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga ambapo utatoa ajira 20,000.

No comments:

Post a Comment