Tuesday 26 July 2016

JK AWACHONGEA WATENAJI CCM KWA JPM

MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya kikwete amewashitaki
watendaji wa Chama kwa Mwenyekiti mpya, Rais Dk. John Magufuli kuwa, hawatoki kwenda kwa wananchi kujua matatizo yao.

Hivyo amemuomba Rais Magufuli kutoacha hali hiyo iendelee ndani ya Chama kwa vile inaweza kukiletea matatizo.

Kikwete alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akifungua mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center, mjini hapa.

Alisema viongozi wengi wa CCM wamekuwa wazito kwenda kwa wananchi na wanachama ili kujua kujua matatizo yao, ikiwemo kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

“Mwenyekiti mtarajiwa, ukae ukitambua hali hii iliyoko ndani ya Chama na ufanye kazi ya ziada kuhakikisha haiendelei, ” alisema.

"Kama wewe hutoki kwenda kwa wananchi kujua matatizo yao, hao wanachama utawapata wapi na nia yetu sisi ni kushawishi watu wengi wajiunge na Chama chetu.

"Watendaji wetu ndani ya Chama hawafanyi vizuri ndani ya chama na nje, hata mali za Chama, ambazo zipo nyingi, bado hazitumiki vizuri katika kukiletea Chama mapato," alisema Kikwete.

Alisema Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana ameonyesha kwa vitendo jinsi gani mtendaji wa Chama anavyotakiwa kufanya, badala ya kukaa ofisini.

Rais mstaafu Kikwete alisema hata baada ya Kinana kupita katika maeneo hayo, bado viongozi wa Chama hawajakwenda tena kuwapitia wananchi.

Aidha, alisema  wanachama wa CCM wamekuwa wagumu kulipa ada zao na hivyo kukifanya Chama kutokuwa na fedha za kutosha kujiendesha.

Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa CCM ina zaidi wa wanachama milioni nane, lakini wanaolipa ada zao ni wachache.

Alisema hali hiyo imekifanya Chama kutegemea ruzuku na kutokana na kuongezeka kwa kura za wapinzani, CCM imekuwa ikipungukiwa ruzuku.

“Ni vyema mali na rasilimali za Chama zikatumika vizuri. Kama pale Dar es Salaam, kuna viwanja vya  Chama zaidi ya 274, lakini ni viwanja 45 tu vyenye hati, ’’ alisema.

Alisema kuna haja ya rasimali hizo za Chama kufuatiliwa kwa karibu ili kiweze kupata mapato kutokana na rasilimali zake.

Kikwete alisema si vyema kwa Chama kuendelea kutegema ruzuku ikitokanayo na idadi ya wabunge na madiwani katika kuendesha shughuli zake, ikiwemo ujenzi wa Chama.

No comments:

Post a Comment