Tuesday 26 July 2016

MAKAMBA ATOBOA SIRI YA KIKWETE KUMTOSA LOWASSA


KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba, ametoboa siri kuwa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliamua kumtosa  rafiki yake kipenzi, Edward Lowassa kwa sababu ya ufisadi.

Amesema hivi sasa Chama kinatoka mikononi mwa kada anayechukukia ufisadi na kinakwenda kwa muasisi wa mahakama ya mafisadi.

Mbali na hilo, amesema kuwa si kweli kwamba Rais Magufuli hakatai ushauri kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali anakataa vimemo, ambapo hata cha kwake alichompelekea cha kumuomba dada yake ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya kilikataliwa.

Makamba alisema hayo jana, wakati akimuombea kura Rais Magufuli kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM na kuongeza kuwa, kiongozi huyo ana kila sifa ya kuwa mwenyekiti wa Chama.

"Chama kinatoka mikononi mwa kada aliyechukia ufisadi na kumtosa rafiki yake kipenzi Lowassa kwa ufisadi," alisema Makamba na kuamsha shangwe na nderemo.

Aliongeza: " Na sasa chama kinatoka kwa muasisi wa ufisadi na kinakwenda kwa muasisi wa mahakama ya mafisadi. "

Aidha, Makamba alisema Chama kinatoka kwa kada anayechukia umasikini na kinakwenda kwa kada, ambaye anaamini kuwa asiyefanyakazi asile.

Aliwapasha wapinzani kuwa Rais mstaafu Kikwete alikuwa anawabatiza watendaji serikalini kwa kutumjia maji, lakini Rais Magufuli atawabatiza kwa moto.

Katibu mkuu huyo mstaafu wa CCM alisema pia kuwa, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, alisema uongozi alipodai kuwa, Rais mstaafu Kikwete hataki kumuachia uenyekiti Rais Magufuli.

Alisema Askofu Gwajima alitaka Rais Magufuli aunde chama chake ama ajitoe CCM kama alivyofanya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye alidai hivi sasa anachezea mchangani Kibaha.

Makamba alisema pengo linaloachwa na Kikwete ndani ya Chama ni kubwa, lakini linazibwa kwa dhahabu.

Alisema baada ya Rais Magufuli kuteuliwa kugombea urais, alialikwa na Kikwete kwenda Morogoro kuhutubia mkutano wa kampeni na akawaambia wananchi kuwa kiongozi huyo anazo kila sifa.

Alisema hashangai kusikia kuwa Rais Magufuli alikataa nafasi ya uenyekiti na kutaka apewe muda zaidi kwa kuwa hata Nabii Mussa alipoambiwa na Mwenyezi Mungu, alikataa na kumuambia ana kigugumizi.

Akinukuu maandiko matakatifu, Makamba alisema: "Isaya alisema, 'Nikasikia sauti ya Bwana ikisema nimtume nani, nikasema mimi hapa nitume bwana."

Alisema Rais Magufuli  alikubali kutumwa na CCM, na ameshafanya kazi nzuri ya kuwatumikia wananchi.

Aliongeza kuwa Rais Magufuli hapaswi kuogopa kwani CCM itatia maneno kwenye kichwa chake naye atasema kwa niaba ya Chama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi, Borafya Silima, alisema Rais mstaafu Kikwete anaondoka kwenye uenyekiti wa Chama akiwa hana doa, hivyo aliwaomba wajumbe wa mkutano huo kumchagua Dk. Magufuli kuwa mwenyekiti.

Alisema Rais Magufuli ni kiongozi muadilifu na muwazi, ambaye hana kundi lolote, hivyo ana kila sifa ya kuwa mwenyekiti.

Borafya alisema kwa niaba ya Wazanzibar wote, wanamuunga mkono Rais Magufuli na wanamuahidi kuwa pamoja naye.

Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe, Deo Sanga alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa kufanyakazi kubwa ya kukijenga Chama.

Alisema Rais Magufuli ni muadilifu na mchapakazi hivyo kwa niaba ya halmashauri kuu anamuombea kura.

No comments:

Post a Comment