Tuesday, 26 July 2016

MTOTO WA KINGUNGE AFUNGUKA, ASEMA WAZEE WALIOJIONDOA CCM WAMEJIDHALILISHA

MTOTO wa mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, Kunje Ngombale Mwiru, ameamua kuvunja ukimya kwa kusema kuwa wazee waliojiondoa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejidhalilisha katika jamii kutokana na kusema uongo na kusambaza chuki.

Kunje amewataka Watanzania kuwa makini na wazee wa aina hiyo, kwani wanaweza kuligharimu taifa kutokana na kueneza siasa za chuki.

Aidha, amewashauri wazee hao kuwa wanapotaka kupumzika siasa, ni vyema wasijiunge na vyama vya upinzani na kuhubiri siasa za chuki kwa maslahi yao binafsi, badala yake wabaki kwenye vyama vyao.

Kunje alisema hayo jana, katika mahojiano maalumu na Uhuru, yaliyofanyika makao makuu ya CCM mjini hapa.

Alisema wazee waliojiondoa ndani ya CCM na kujiunga na vyama vya upinzani walikuwa wakizungumza uongo majukwaani na kwamba Watanzania waliwachambua na kuwadharau.

Aliwataka wazee waliobaki ndani ya Chama, wajiepushe na ushawishi wa uroho wa madaraka, kwani ni wakati wao wa kutafuta thawabu kwa Mwenyezi Mungu.

Akizungumzia vyama vya upinzani, Kunje aliwataka wajipange kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020, na kwamba katika uchaguzi uliopita, wapinzani walikuwa hawana sababu ya kushinda.

“Wapinzani mtaji wetu ulikuwa wa ufisadi, lakini baada ya mafisadi kujiunga na vyama vya upinzani, tulikosa hoja za kuzungumza,” alisema.

Kunje, ambaye katika uchaguzi uliopita aligombea ubunge katika Jimbo la Mkuranga kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, alisema wananchi wamechoshwa na siasa za maigizo zinazofanywa na wapinzani.

Alisema baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, wabunge wanaotoka vyama vya upinzani hawana kitu walichofanya tokea walipoingia bungeni zaidi ya kushiriki migomo isiyokuwa na tija kwa wapiga kura wao.

“Hata hao wabunge, ambao tumepata wapinzani, hatujaona chochote walichofanya zaidi ya kujiziba midomo na kutoka bungeni,” alisema.

Aliongeza: ”Kwa vile wapinzani tumekosa hoja za msingi za kuibana serikali, basi tutaendelea kuisoma namba na kwa msingi huo hatuwezi kufanana na wenzetu wa CCM.”

Kunje alisema CCM ni chama cha kupigiwa mfano na vyama vingine vya upinzani hapa nchini na nje ya nchi, kutokana na umoja na mshikamano uliomo katika Chama hicho.

Alisema viongozi wa CCM hawana tama ya kung’ang’ania madaraka kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani, ambapo viongozi wa vyama vya upinzani wanajifanya miungu watu.

Kunje alisema ataendelea kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli, kama alivyofanya kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

“Rais Magufuli, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM, ni mchapakazi, mtendaji mzuri kama alivyokuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, hivyo nina imani naye kubwa kuwa ataleta mabadiliko makubwa hapa nchini,” alisema.

Aliwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli na serikali yake ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuleta maendeleo nchini.

Aidha, alisema Kikwete katika utawala wake alifanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, huduma za afya na sekta ya elimu.

“Rais Kikwete wakati wa utawala wake alifanya mambo mengi mazuri, ikiwa ni pamoja na kutuletea mgombea bora, ambaye ni Dk. Magufuli, hivyo tutaendelea kumkumbuka daima,” alisema.

Alisema pamoja na kashikashi iliyofanywa na wazee waliohama ndani ya CCM, Rais Kikwete, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CCM, aliweza kusimama imara na kukisimamia Chama na hatimaye kushinda katika uchaguzi mkuu.

Kunje alisema mshikamano uliopo ndani ya CCM ni dhahiri kwamba haiwezi kuondoka madarakani kwa miaka mingi ijayo, kutokana na upinzani kufanya maaigizo badala ya siasa.

Alisema wananchi wamechoshwa na siasa za maigizo zinazofanywa na vyama vya upinzani, hivyo katika uchaguzi mkuu uliopita baada ya kubaini maigizo yaliyokuwa yakifanywa na wapinzani, waliamua kuichagua CCM na kupata ushindi mkubwa.

Kunje alisema alianzia siasa akiwa  CHADEMA, lakini aliondoka katika chama hicho baada ya kuwakaribisha mafisadi waliokuwa wakiwasema kila siku.

Mwanasiasa huyo alisema vyama vya siasa vingi ni vya mifukoni mwa watu wachache na vimekosa sera na mwelekeo madhubuti wa uwezo wa kuongoza.

“Hivi vyama vya upinzani vilivyopo vingi ni vya mifukoni tu, haviwezi kushindana na CCM ambayo ni taasisi na iko imara wala haiyumbi,” alisema.


No comments:

Post a Comment