MWENYEKITI wa Chama cha UDP, John Cheyo amewashauri wenyeviti wenzake wa vyama vya siasa kuwa, Chama cha Mapinduzi (CCM) ni vigumu kukitoa madarakani kutokana na ubora wake.
Aidha, wanachama wawili waliotoka CCM mwaka jana na kujiunga na vyama vya upinzani, akiwemo Fred Mpendazoe na Mgana Msindai wametangaza kurudi kundini kutokana na kuchoshwa mwenendo wa upinzani.
Cheyo alisema hayo jana, alipokuwa akitoa salamu kwa viongozi na wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center, mjini hapa.
Alisema ni vyema vyama vingine vya upinzani kulitambua hilo na kama wanalitambua, wanatakiwa kutofanya siasa za kitoto, ikiwemo kususia bunge kama njia ya kuitoa madarakani CCM.
“Huwezi kuing’oa CCM kwa kufanya siasa za kitoto za kususia bunge, ni lazima utambue kuwa wachache watasikilizwa na wengi wataamua, sasa wewe unatoka bungeni huwezi kuing’oa CCM,’’ alisema.
Mwenyekiti huyo sz UDP alisema katika uchaguzi mkuu uliopita, CCM ilitikisika kidogo, lakini imejitahidi na kupata ushindi wa kishindo.
"Sasa tunakiomba chama hiki kihakikishe hakitikisiki tena na kama kikitikisika, basi mtuambie tujiandae kwani mti mkubwa ukianguka na hata sisi tuatatikisika sana,’’ alisema.
MPENDAZOE AJUTA
Kwa upande wake, Fred Mpendazoe akitoa salamu kwa wajumbe, alisema kuwa amerudi CCM ambako ndipo kwa baba na mama.
Mpendazoe alisema amerudi kwenye Chama alikotoka, kutokana na kukujua vizuri kuliko alikokuwa amekwenda.
Alisema CCM imeonyesha ukomavu mkubwa wa kidemokrasia, hasa wakati wa kupata wagombea wa nafasi ya urais mwaka jana, kwa kuwa na wagombea 38, lakini waliweza kumpata mmoja bila kufarakana.
Alisema inashangaza kuona chama kama CHADEMA kikiwa kinapita kila kona ya nchi kuwa kinatangaza demkrasia wakati mgombea wake anapatikana kwa watu watatu kukutana kwenye chumba na kuamua.
“Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema kama hakutakuwa na mabadiliko ndani ya CCM , wanachama watatoka na kwenda kuitafuta nje ya CCM. Lakini hata (Marehemu Nelson) Mandela alisema ukitaka kufanya mabadiliko ni lazima wewe mwenyewe ubadilike, sasa hawa wenzetu CHADEMA hawana mabadiliko, lakini wanataka mabadiliko nje ya chama,’’ alisema.
Alisema alipokuwa CHADEMA, alikuwa akitoa mawazo yake, lakini wamekuwa wakipinga na mara nyingi sifa ya kuwa kiongozi katika chama hicho ni kuwa mkorofi dhidi ya serikali.
"Niliulizwa nimekaa rumande mara ngapi, nikasema bado, nikaulizwa nimepigwa mabomu mara ngapi, nikasema bado, umeandamana mara ngapi, nikasema sijawahi , hii inaonyesha kama si mkorofi, huwezi kuingia huko na kupata sifa ya kuwa kiongozi,’’ alisema.
Mpendazoe alisema pia utayari wa Rais John Magufuli umeonyesha mabadiliko makubwa ndani ya serikali kwa kushughulika na malalamiko mengi ya wananchi.
"Sikuona sababu ya kuendelea kuwa nje ya CCM huku kila kitu ambacho tulikuwa tukilalamikia kufanyiwa kazi na Magufuli, tena kwa kasi kubwa, nimerudi CCM,’’ alisema.
MGANA MSINDAI AUNGAMA
Kwa upande wake, Msindai alianza kwa kuomba msamaha kwa kutoka CCM na kusema kuwa alikuwa safari kidogo nje ya CCM, lakini hakukaliki.
“Naomba msamaha wanachama wote wa CCM kwa kuondoka CCM na mimi nawasamehe wote walionikosea, tusamehane. Nilipokwenda ni kama mahabusu, tukae pamoja tuijenge CCM yetu,’’ alisema.
Alisema Rais Magufuli ni kama mdudu anayeitwa jongoo, ambaye ana miguu mingi hivyo matendo ya rais huyo ni sawa na jongoo kwa kugusa kila eneo, ambalo lilikuwa linapigiwa kelele na wananchi.
"Nilikuwa mwana mpotevu, lakini sasa nimerudi kwa baba na mama, wazazi wangu, ambao ni CCM na sasa akiwa mwenyekiti wadokozi wote wa ndani ya serikali na chama muda wao unahesabika,’’ alisema.
Mpendazoe alimmwagia sifa Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana kwa kazi nzuri ya kupita nchi nzima na kusikiliza kero za watanzania na kuzifanyia kazi.
MREMA ALIPUKA
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema Rais Magufuli ni rais wa watu kwani hachagui chama cha kufanya naye kazi, ndiyo maana alimchagua yeye kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Palore.
Alisema yeye binafsi alipopigiwa simu na rais ya uteuzi wake, hakuamini na ndipo alipomuita mkewe ili awe shahidi.
Mrema alisema yeye kama mwenyekiti, aliamua kufanya biashara na Rais Magufuli baada ya kumuona kuwa ni rais wa watu, hivyo hakuweza kukataa uteuzi huo.
"Rais alipita kwangu akielekea Mwanga, alikuwa kishapita zaidi ya kilometa tano, lakini alisimamisha msafara wake na kurudi kuja kunisalimia. Sasa kwanini nisimuunge mkono?
"Hawa wapinzani wenzangu wanasema uteuzi wangu ni kutokana na ukibaraka wa CCM, sasa mimi namuuliza Mbatia, wakati Rais Kikwete anamteua kuwa mbunge, alikuwa chama gani? Yeye ni CCM?’’ Alihoji.
Mwenyekiti huyo alisema haombi radhi kwa mtu yeyote kuhusiana na kumuunga mkono Rais Magufuli.
Alisema yeye binafsi kama kiongozi wa chama cha upinzani, anashangazwa na kitendo cha kambi ya upinzani kususia vikao vya bunge.
No comments:
Post a Comment