Tuesday 26 July 2016

KINANA: SIWEZI KULEWA SIFA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ameahidi kuwa hatalewa sifa, badala yake atatumia sifa katika kuongeza juhudi za kufanyakazi ya kukijenga Chama.

Kinana alisema hayo juzi, wakati akitoa neno la shukrani baada ya kuteuliwa tena kuendelea na nafasi yake, katika mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center (DCC), mjini hapa.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, aliomba ridhaa ya wajumbe wa mkutano huo kumkubalia pendekezo lake la kumtaka Kinana na sekretarieti yake kuendelea na nyadhifa hizo hadi atakapoamua vinginevyo.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kinana kuwasilisha barua aliyoiandika juzi, akiomba kujiuzulu pamoja na sekretarieti yake ili kumpa nafasi mwenyekiti kufanya uteuzi mpya.

Kutokana na uamuzi huo wa Rais Magufuli, wajumbe wa mkutano huo waliridhia kwa kauli moja pendekezo lake.

Akizungumza wakati akitoa neno la shukrani kwa Mwenyekiti wa Chama na wajumbe wa mkutano huo, Kinana alisema atafanyakazi kwa moyo mmoja na kamwe hatalewa sifa, badala yake atatumia sifa katika kuongeza juhudi za kufanyakazi.

“Nakushukuru ndugu mwenyekiti kwa kuniteua tena. Naahidi kuwa sitalewa sifa bali nitatumia sifa kuongeza juhudi za kufanyakazi,” alisema.

Aliongeza: “Imani huzaa imani, hivyo naahidi kufanyakazi kwa bidii, uadilifu na nitatekeleza maagizo yote nitakayoelekezwa.”

Kinana, ambaye alijipatia sifa kubwa ya utendaji uliotukuka katika kipindi cha awamu ya nne, alimshukuru Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyomuonyesha ya kutaka kuendelea kufanya naye kazi.

Alisema maombi yake ya kuomba kujiuzulu yamegonga mwamba, baada ya Rais Magufuli kumkatalia, hivyo aliahidi kumpa ushirikiano wa hali na mali kipindi chote atakachokuwa mtumishi na hata akiwa nje ya utumishi.

“Rais Magufuli, ambaye sasa ni mwenyekiti wetu wa Chama, amenikatalia kujiuzulu na kunitaka niendelee kufanya naye kazi, hivyo nitampa ushirikiano wa hali na mali na nitaendelea kuchapakazi kwa juhudi na maarifa zaidi,” alisema Kinana na kushangiliwa na wajumbe wote wa mkutano huo.

Alimshukuru mwenyekiti mstaafu, ambaye pia ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kumteua kushika nafasi hiyo wakati wa utawala wake.

Kinana alisema Kikwete alimuamini na walifanyakazi vizuri ya kukijenga Chama na kwamba muda wote aliohitaji kumuona, hakukuwa na kikwazo.

“Kila nilipotaka kumuona Rais Kikwete, milango ilikuwa wazi, hakukuwa na kikwazo chochote hata pale nilipokuwa nampigia simu, hakusita kupokea simu yangu,” alisema.

Aliongeza: “Hata zile ziara zangu za mikoani, Rais Kikwete alikuwa akinitia moyo sana. Alinipa ushirikiano wa kila aina na nilipokuwa nampa ushauri, hakusita kunisikiliza na muda mwingine alipoona unafaa, alikuwa anaufanyia kazi kwa haraka.”

Kinana, ambaye alijizolea umaarufu kutokana na kukirudisha Chama kwa wananchi na kujenga umoja na mshikamano, alisema Kikwete ni kiongozi muungwana, ana roho mzuri, muadilifu na mchapakazi.

Aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kuonyesha imani kubwa kwake na kumpa ushirikiano kipindi chote alipokuwa anatekeleza majukumu yake.

No comments:

Post a Comment