Monday 24 October 2016

PUUZENI PROPAGANDA ZA WAPINZANI- VUAI

NA IS-HAK OMAR, ZANZIBAR

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka wanachama wake na wananchi kwa ujumla, kupuuza na kudharau propaganda zinazotolewa na baadhi ya vyama vya upinzani  kwa lengo la kuwapotezea muda.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tafauti na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai ali Vuai, mkoa wa Kusini Pemba, jana, alipokutana na kuzungumza na Kamati ya Siasa ya Mkoa huo pamoja na wanachama wa CCM Tawi la Vitongoji.

Naibu Katibu Mkuu alisema wapinzani wanajua fika kuwa hakuna na wala hakutakuwa na uchaguzi mkuu mwingine Tanzania Bara  na Zanzibar, hadi mwaka 2020 na wanachokifanya sasa ni kuendeleza siasa zisizokuwa na maslahi kwa familia maskini za Wazanzibar.

Alisema wanasiasa wanatakiwa kuwa wazalendo na kusoma alama za nyakati kwa kufanya siasa zinazowahamasisha wananchi wafanye kazi kwa bidii za kujiletea maendeleo, badala ya kuwapotosha.

“Wana-CCM na wananchi kwa ujumla tumemaliza uchaguzi wa marudio, sasa tufanye kazi za kujiongezea kipato na kujiletea maendeleo huku tukisubiri kufanya siasa katika uchaguzi ujao na si wakati huu.

"Pia, tunajua kuwa wapinzani, hususan CUF kwa upande wa Zanzibar tumewadhibiti kila upande na hawana pa kutokea, ndio maana wanahangaika kila kona ya dunia kuomba msaada ili kurudi katika ushindani wa kisiasa, jambo ambalo haliwezekani kwa sasa,”alisema.

Vuai aliwaomba  wana-CCM kutumia uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika mwakani, kupata viongozi imara wa Chama wenye uwezo wa kuendeleza ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwapongeza wabunge, wawakilishi na madiwani wa CCM Pemba, kwa kuwa karibu na wananchi katika  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment