Monday 24 October 2016

MUUGUZI CHUNYA ATUMBULIWA NA KUKAMATWA NA POLISI



NA SOLOMON MWANSELE, CHUNYA

SERIKALI wilayani Chunya, imemsimamisha kazi muuguzi mkunga wa Hospitali ya wilaya hiyo, Patricia Chisoti, kwa tuhuma za kumtelekeza mjazito aliyefika hospitalini hapo usiku ili kujifungua.

Hali hiyo ilisababisha mjamzito huyo aliyejitambulisha kwa jina la Maria Mwaipasi, kushindwa kupata huduma kwa muda mwafaka usiku huo, hadi asubuhi alipofanikiwa kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji, lakini mtoto akafariki dunia baadaye.

Tukio hilo lilimfanya Mkuu wa wilaya hiyo, Rehema Madusa na wanawake wengine waliokusanyika hospitalini hapo, kujikuta wakiangua vilio, baada ya kumsikia mama wa mtoto huyo akieleza hali halisi ilivyokuwa.

Patricia, anatuhumiwa kusababisha kifo hicho Septemba 4, mwaka huu, baada ya kushindwa kumhudumia Maria, aliyefikishwa hospitali hapo usiku, akiwa ameshikwa na uchungu wa kujifungua.

Mkuu wa Wilaya, Rehema, ambaye alifika hospitalini hapo akiwa ameongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, baada ya kusikia maelezo ya Maria, alimuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kumchukua mtuhumiwa Patricia na kumfungulia mashitaka.

“Wakati serikali inapambana kupunguza vifo vya wajawazito na watoto, bado kuna watumishi kama Patricia, wanarudisha nyuma jitihada hizo pamoja na kupuuza na kukaidi misingi ya kiutumishi,” alisema Rehema.

Alisema jambo hilo ni baya kwa kuwa ni uuaji, kwani kwa vyovyote Maria kama angepata huduma kwa wakati kutoka kwa muuguzi huyo, igesaidia kuokoa maisha ya mtoto.

Mkuu huyo wa wilaya alisema muuguzi huyo alishindwa kufanya hilo, badala yake alimjibu Maria kuwa, amechoka na anahitaji kupumzika, wakati akitambua wazi kuwa mama huyo alikuwa kwenye uchungu.

Awali, akisimulia jinsi hali ilivyokuwa alipofika hospitalini hapo, Maria alisema alifika hospitalini hapo usiku, akiwa amesindikizwa na wifi yake huku akiwa na hali mbaya ya uchungu.

Maria alisema alipofika alishindwa kupewa msaada wowote na hata alipogonga mlango zaidi ya mara tatu kumuita muuguzi aliyekuwepo zamu, hakuna aliyejitokeza kumfungulia ili kumsaidia zaidi ya wifi yake aliyekuwa amebeba beseni la nguo kwa ajili ya mtoto.

“Baadaye muuguzi Patricia alikuja na kumuamuru wifi yangu anipe nguo na nikamueleza nesi nimetingwa, nimeshindwa hata kunyanyua mguu wangu, lakini namshukuru Mungu nikageuka kwa haraka na kumpokea wifi yangu beseni la nguo,”alisema Maria huku akitokwa na machozi.

Aliongeza kuwa alipoingia chumba cha kujifungulia, alimuomba tena msaada muuguzi Patricia, ambaye alimuangalia kwa dharau huku akimtaka mama huyo kujitandikia kitanda, ambapo ilimlazimu kutekeleza hilo huku akiwa na uchungu mkali.

Maria, aliyekuwa anatoa ushuhuda huo huku akibubujikwa na machozi, aliongeza kuwa baada ya kumaliza kutandika, alishindwa kupanda kitandani, kwani inaonyesha muda huo mtoto alikuwa yupo njiani kutoka na hata nguvu ya kusukuma ikawa inafika, lakini akashindwa.

“Kwa kweli nilipanda kitandani kwa ujasiri, nikalala. Muuguzi Patricia aliniuliza ‘gloves’ zipo wapi, nikamjibu zipo hapo, akachukua, akavaa na kisha kunipima, akaniambia lala ubavu, akaondoka na  nikasubiri kwa muda mrefu huku muuguzi huyo akiwa ametoka nje na kunifungia mlango,”alisema.

Aliongeza kuwa baadaye akiwa katika kuhangaika, chupa ya maji ilipasuka, akaanza tena kumuita muuguzi Patricia, ambaye alimjibu anampigia kelele.

Maria alisema Patricia alifika na kumuuliza anataka amsaidiaje, ambapo alimjibu ametingwa na uchungu, lakini alimjibu mbona ana haraka sana na yeye kujibu inaonyesha mtoto yupo karibu kutoka kwani anasikia maumivu makali.

“Nililala pale kitandani kwa muda mrefu huku Patricia akiwa hanipi msaada wowote na kutokana na muda kwenda, nilianza tena kupiga kelele za kuomba msaada, ndipo alipotokea tena na kunijibu kwa nini namsumbua kwani na yeye ni binadamu, anahitaji kupumzika,” alisema mama huyo na kuangua kilio.

Aliongeza kuwa ilipofika asubuhi, ndipo walitokea madaktari wawili ambapo baada ya kumuona hali yake ilivyo, walilazimika kumfanyia upasuaji na kufanikiwa kumtoa mtoto, ambaye alikuwa amechoka na hivyo kulazimika kuwekekwa kwenye mashine, lakini alifariki baadaye.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli, alisema akiwa muajiri na msimamizi wa watumishi wote, anatambua watumishi wana mikatana ya kazi waliyoingia na pia kila mtumishi amesomea kada aliyopo.

Sophia alisema wapo watumishi waadirifu, lakini kuna wachache mfano wa Patricia, wanaoichafua, hivyo anamsimamisha kazi huku taratibu za uchunguzi wa awali zikianza kuchukuliwa mara moja.

Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Saasita Shabani, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, atahakikisha wanajipanga vyema ili tukio kama hilo lisije kujirudia tena hospitali hapo.

Patricia alipoombwa na waandishi wa habari kuzungumzia chochote juu ya tuhuma hizo, alijibu kwa mkato kuwa hana cha kuzungumza na kuondoka kuelekea wodini, ambapo askari polisi walimfuata kumchukua na kwenda naye kituo cha polisi cha wilayani humo.

No comments:

Post a Comment