Monday 24 October 2016

SIMBACHAWENE: SIJASEMA MUWAKAGUE WALIMU, FUATILIENI MAFUNZO YANAYOTOLEWA KWA WANAFUNZI

NA WILLIAM SHECHAMBO, DODOMA

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene, ametoa ufafanuzi juu ya agizo alilolitoa hivi karibuni kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kupita shuleni kwamba, lililenga kuangalia maendeleo ya wanafunzi.

Agizo hilo alisema lilieleweka vibaya na baadhi ya viongozi hao, ambao walidhani liliwataka kukagua ufundishaji wa walimu madarasani katika shule zilizo kwenye maeneo yao ya utawala.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita na wananchi kwenye vijiji vya Mungui, Kidenge katika Kata ya Pwaga na Ilamba, Mtamba Kata ya Rudi wilayani Mpwapwa, Waziri Simbachawene alisisitiza kuwa ni lazima viongozi hao kujenga utamaduni wa kupita madarasani kuona kama wanafunzi wanapata elimu kama ilivyokusudiwa na serikali.

“Sikusema wawakague walimu, bali waangalie je wanafunzi wanafundishwa? Na kama wanafundishwa je, wanafundishwa vizuri? Na kuangalia kama wanafunzi wanajua kusoma na kuandika vizuri,” alifafanua.

Waziri Simbachawene aliongeza kuwa, kusoma na kuandika hakuhitaji mtu aliyesomea taaluma hiyo kuweza kumjua mtoto kama anajua kusoma na kuandika.

“Hili ni jukumu letu sote. Hivi karibuni nilikwenda katika shule moja na kukuta watoto wa darasa la sita, walimu wapo wanane, lakini watoto wale hawajui kusoma wala kuandika,”alisema.

Alisema kuanzia Agosti, mwaka huu, serikali imekuwa ikitoa posho kwa walimu wakuu wa shule za msingi, wakuu wa shule za sekondari na wakaguzi wa elimu kata, wamekuwa wakipewa sh. 200,000, kila mwezi kwa ajili ya kuwapa motisha.

Wakati huo huo, kwenye ziara hiyo aliyoitumia kutembelea shule ya msingi ya Maswala, iliyoko kijiji cha Maswala, kata ya Pwaga, wilayani Mpwapwa, waziri huyo alibaini upungufu mkubwa shuleni hapo.

Upungufu huo ni uwepo wa madarasa matatu ya kusomea, nyumba moja ya mwalimu na upungufu mkubwa wa madawati, ambapo uongozi wa halmashauri hiyo ulilazimika kuwahamishia wanafunzi kuanzia darasa la nne hadi la saba katika shule ya msingi ya Pwaga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Donath Sesine Ng’hwenzi, alisema kuanzia sasa halmashauri hiyo haitakuwa tayari kupitisha fedha katika mradi, ambao ama umetekelezwa vibaya au haujakamilika.

No comments:

Post a Comment