JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma, limemtaka dereva wa mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, anayejulikana kwa jina la Adam, aripoti katika ofisi ya upelelezi mkoa au Makao Makuu ya Upelelezi mkoa wa Dar es Salaam, kwa ajili ya kuhojiwa.
Aidha, jeshi hilo limemtaka Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Vicent Mashinji, naye aripoti katika ofisi hizo ili ahojiwe, baada ya kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akidai kuwa, anawafahamu watu waliomshambulia kwa risasi mbunge huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP, Gilles Muroto, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, wanamtaka Adam afike polisi kwa kuwa ni shahidi muhimu katika tukio la kushambuliwa Lissu na ndiye aliyekuwa akiendesha gari lake wakati wa tukio hilo.
Alisema wanashangaa kuona hadi sasa Adam hajaripoti polisi kwa ajili ya kutoa taarifa za tukio hilo wakati ndiye mtu pekee aliyekuwa na Lissu wakati akishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
"Jeshi la Polisi linamtaka Adam, ambaye alikuwa naye (Lissu) siku ya tukio, popote alipo, ajitokeze kwa kufika Polisi Dodoma bila kukosa au Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam, ili aweze kutoa maelezo yake kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa ndiye aliyekuwa pamoja na majeruhi wakati wa tukio,"alisema Kamanda Muroto.
Aliongeza kuwa Adam ndiye mwenye siri za tukio hilo, hivyo kutoweka kwake au kujificha ni kosa la jinai na kama kuna mtu au watu wanaomficha, wanatenda kosa la jinai, hivyo wamfikishe polisi bila kukosa kwa kuwa ni shahidi muhimu katika upelelezi.
"Huyu bila shaka anazo siri za tukio hili, anafahamu nini kilichotokea, lakini hataki kusema kitu. Kukalia ushahidi ni kosa la kiuhalifu,"alisisitiza Kamanda Muroto.
Kuhusu Dk. Mashinji, alisema alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi, akidai kuwa, anawafahamu watu waliomshambulia Lissu, hivyo anapaswa kuripoti polisi ili aweze kuwasaidia kupata taarifa hizo.
Kamanda Muroto alionya kuwa, tukio la kushambuliwa kwa Lissu halipaswi kugeuzwa kuwa mtaji wa kisiasa na kuwataka wananchi waliache jeshi la polisi lifanyekazi yake.
Alisema kama jeshi hilo liliweza kutekeleza vyema majukumu yake katika matukio yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo ya Kibiti mkoani Pwani, Mbande na Kongowe mkoani Dar es Salaam, haoni kwa nini lishindwe kuwakamata na kuwashughilikia waliomshambulia Lissu.
"Tunatoa wito kwa wanasiasa, waache kuwachochea wananchi kwa sababu hilo ni kosa la jinai. Wanaofanya hivyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria," alisema.
Vilevile, aliwaonya watu wanaosambaza taarifa za uzushi kuhusu tukio hilo kwa kusema kuwa, hilo nalo ni kosa kisheria na kwamba, tayari jeshi la polisi limeshaanza kuwasaka ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa Kamanda Muroto, hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, isipokuwa wamekamata magari manane aina ya Nissan, yenye rangi nyeupe, yanayofanana na gari lililotumiwa na watu waliomshambulia Lissu. Alisema wamiliki wa magari hayo wameshahojiwa.
Alisema wameshaanza kuyafanyia uchunguzi magari hayo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi zingine, kuhusiana na tukio la kujeruhiwa kwa risasi mbunge huyo.
Pia, alisema wameshaihoji familia ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ambayo ilikuwa ya kwanza kushuhudia tukio hilo na kutoa taarifa polisi, kutokana na nyumba yao kuwa jirani na ya Lissu na ndio iliyomtoa kwenye gari lake na kumfikisha hospitali.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, wahalifu walitumia silaha aina ya SMG/SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa eneo la tukio. Alisema Lissu alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake lenye namba za usajili T216 DHH aina ya Toyota Land Cruiser rangi nyeusi, likiendeshwa na Adam.
Alisema polisi mkoani Dodoma kwa kushirikiana na timu kutoka makao makuu ya upelelezi Dar es Salaa, wanaendelea kufanya upelelezi wa kina ili kuwabaini waliohusika katika tukio hilo na taarifa zitatolewa mapema.
Ametoa wito kwa wananchi wenye taarifa zozote kuhusu tukio hilo, kuripoti polisi bila kuwa na woga ili waweze kulisaidia jeshi hilo kuwasaka na kuwakamata waliohusika kumshambulia mbunge huyo.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, limepiga marufuku uchangiaji damu unaohamasishwa na CHADEMA kwa wanachama wake mkoani hapa kwa madai kuwa hizo ni mbinu za kisiasa za kuchochea ghasia.
Alisema haoni ni kwa nini CHADEMA watake kuchangia damu kipindi hiki baada ya mbunge wao kushambuliwa kwa risasi huku wakiwa wamevalia sare za chama chao, wakati wangeweza kufanya hivyo kabla ya tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo bungeni mjini hapa juzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Lissu alishambuliwa kwa risasi Alhamisi iliyopita, saa saba mchana, akiwa anarejea nyumbani kwake Area D kwa mapumziko, baada ya bunge kusitishwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Alisema alipofika nyumbani kwake, kabla hajashuka kwenye gari lake, watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari jeupe aina ya Nissan, ambalo namba zake hazikuweza kutambulika, walianza kumshambulia kwa risasi kadhaa.
Alimkariri Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Giles Muroto, akisema kuwa, risasi zilizotumika ni kati ya 28 na 32, ambazo zilimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Alisema risasi moja kati ya hizo ilimpata mkononi, mguuni mbili na zingine mbili tumboni. Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walikimbia.
Ndugai alisema baada ya tukio hilo, Lissu alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu. Alisema alipelekwa hospitali kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika Dk. Tulia, kutokana na kuishi naye jirani.
Kwa mujibu wa Spika Ndugai, baada ya kufikishwa hospitali, aliingizwa moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji ili kuzuia damu kuendelea kutoka katika majeraha aliyokuwa ameyapata.
Alisema upasuaji huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Asubisye Mpoki, akisaidiwa na madaktari bingwa wa Mkoa wa Dodoma. Baada ya upasuaji huo, ilielezwa kuwa hali yake inatengemaa na anaweza kusafirishwa kwa matibabu zaidi.
Spika Ndugai alisema saa 4.30 usiku wa siku hiyo, ilifika ndege ya Kampuni ya Flying Doctors na kuondoka na mgonjwa saa sita usiku, kwenda Nairobi, Kenya.
Alisema katika safari hiyo, Lissu aliambatana na Mbowe, Mchungaji Peter Msigwa, mkewe, madaktari wawili kutoka Kampuni ya Flying Doctors.
Aidha, alisema Katibu Mkuu Wizara ya Afya, alishauri daktari aliyemfanyia upasuaji Lissu, kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, naye aambatane na mgonjwa na kumkabidhi kwa madaktari wa Agha Khan.
Hadi ya Lissu imeelezwa kuwa ni nzuri, akiwa amerejewa na fahamu na kuweza kuwatambua watu wanaomtembelea hospitalini hapo, lakini bado yupo kwenye chumba cha uangalizi maalumu baada ya kufanyiwa upasuaji kwa saa saba.
No comments:
Post a Comment