Friday, 8 September 2017

KAMATI YA BUNGE KUKUTANA NA VYOMBO VYA USALAMA



SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, ameiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, kukutana kwa ajili ya kujadili matukio ya utekaji nyara, yaliyoanza kushamiri nchini.

Ndugai ameiagiza kamati hiyo kukutana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kujadili kuhusu vitendo hivyo na kisha kuiwasilisha ripoti yao bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge.

Agizo hilo la Spika Ndugai lilitokana na mwongozo ulioombwa na mbunge wa Nzenga Magharibi (CCM), Hussein Bashe kwa kutumia kanunu ya 47, kifungu cha kwanza na ya pili.

Katika mwongozo huo, Bashe alisema katika siku za hivi karibuni, kumetokea matukio ya utekaji nyara, ikiwepo kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, ambapo bunge na serikali zimeshatoa kauli.

Aliyataja matukio mengine kuwa ni kutekwa nyara kwa Ben Saanane wa CHADEMA, msanii Roma Mkatoliki, ambapo licha ya vyombo vya ulinzi kufanya upepelezi, hakuna hatua zilizochukuliwa.

Aidha, alisema mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliwahi kutishiwa kwa bastola hadharani, lakini muhusika hadi sasa hajachukuliwa.

Hivyo alimuomba Spika Ndugai aiagize kamati hiyo kukutana na vyombo vinavyohusika kusimamia masuala ya ulinzi na usalama ili kujadili matukio hayo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa.

Alisema iwapo hilo litawezekana, ripoti ya kamati hiyo iwasilishwe bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, ombi ambalo lilikubaliwa na idadi kubwa ya wabunge.

Kufuatia wabunge wengi kuunga mkono mwongozo huo, Spika Ndugai aliiagiza kamati hiyo, ambayo mwenyekiti wake ni mbunge Adadi Rajabu, kukutana jana mchana kujadili suala hilo kabla ya kukutana na mamlaka zinazohusika kusimamia masuala ya ulinzi na usalama.

No comments:

Post a Comment