Friday, 8 September 2017

NDUGAI AELEZA SABABU ZA LISSU KUPELEKWA KENYA, BUNGE LAMCHANGIA MILIONI 43


BUNGE limesema uamuzi wa kumpeleka mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Aga Khan nchini Kenya, baada ya kujeruhiwa kwa risasi, umetokana na matakwa ya familia yake na chama hicho.

Limesema ofisi yake ilishajipanga kumuhamishia mbunge huyo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, ikiwa ni pamoja na kumkodishia ndege, lakini familia yake ilikataa.

Aidha, bunge limemchangia Lissu sh. milioni 43, kwa ajili ya kusaidia matibabu yake huko Kenya, zikiwa ni makato ya nusu ya posho wanayolipwa kwa siku moja. Fedha hizo ni sh. 110,000 kwa kila mbunge. Kwa sasa bunge lina wabunge 391.

Akizungumza na wabunge kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, mjini hapa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kwa mujibu wa taratibu za bunge, mbunge anapopatwa matatizo yanayohitaji matibabu, anapaswa kugharamiwa kwa kupatiwa matibabu Muhimbili au kwenye Hospitali ya Apolo, India.

"Hivyo, ofisi ya bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliagiza ndege, ambayo ilifika Dodoma, saa 10.30 jioni, kwa ajili ya kumchukua mgonjwa na kumpeleka Hospitali ya Rufaa Muhimbili kwa matibabu zaidi kama taratibu zetu za kawaida zilivyo. 

"Hata hivyo, baada ya mashauriano, familia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (Freeman Mbowe), walishauri kuwa ni vema mgonjwa apelekwe Hospitali ya Agha Khan, Nairobi,"alisema Spika Ndugai.

Alimnukuu Mbowe akisema kuwa, hawana shaka na uwezo wa madaktari wa hapa nchini, ikiwemo Muhimbili, kwa sababu walimsaidia kwa kiasi kikubwa kupata nafuu na wanafarijika kwa hilo, lakini wameamua akatibiwe Kenya.

"Tunawaomba Watanzania walielewe hili, tulishajiandaa kugharamia matibabu yake, lakini tuliheshimu uamuzi wa familia yake," alisisitiza Spika Ndugai.

Aliwalaumu baadhi ya wabunge kwa kuandika habari potofu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu tukio la kupigwa risasi Mbowe, lakini alimpongeza Mbowe kwa kuwataka wananchi wawe na subira na kuviacha vyombo vinavyohusika kuchunguza tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Spika Ndugai alisema Lissu alishambuliwa kwa risasi juzi, saa saba mchana, akiwa anarejea nyumbani kwake Area D kwa mapumziko, baada ya bunge kusitishwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Alisema alipofika nyumbani kwake, kabla hajashuka kwenye gari lake, watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari jeupe aina ya Nissan, ambalo namba zake hazikuweza kutambulika, walianza kumshambulia Lissu kwa risasi kadhaa.

Alimkariri Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Giles Mloto, akisema kuwa, risasi zilizotumika ni kati ya 28 na 32, ambazo zilimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Alisema risasi moja kati ya hizo ilimpata mkononi, mguuni mbili na zingine mbili tumboni. Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walikimbia.

Ndugai alisema baada ya tukio hilo, Lissu alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu. Alisema alipelekwa hospitali kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika Dk. Tulia, kutokana na kuishi naye jirani.

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, baada ya kufikishwa hospitali, aliingizwa moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji ili kuzuia damu kuendelea kutoka katika majeraha aliyokuwa ameyapata. 

Alisema upasuaji huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Asubisye Mpoki, akisaidiwa na madaktari bingwa wa Mkoa wa Dodoma. Baada ya upasuaji huo, ilielezwa kuwa hali yake inatengemaa na anaweza kusafirishwa kwa matibabu zaidi.

Spika Ndugai alisema saa 4.30 usiku, ilifika ndege nyingine ya Kampuni ya Flying Doctors na kuondoka na mgonjwa saa sita usiku, kwenda Nairobi, Kenya.

Alisema katika safari hiyo, Lissu aliambatana na Mbowe, Mchungaji Peter Msigwa, mkewe, madaktari wawili kutoka Kampuni ya Flying Doctors. 

Aidha, alisema Katibu Mkuu Wizara ya Afya, alishauri daktari aliyemfanyia upasuaji Lissu, kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, naye aambatane na mgonjwa na kumkabidhi kwa madaktari wa Agha Khan.

Spika Ndugai alisema jana asubuhi, kulifanyika kikao cha pamoja cha Kamati ya Uongozi na Tume ya Utumishi wa Bunge, ambapo pamoja na mambo mengine, walikubaliana wabunge wote kuchangia  nusu ya posho ya kikao kimoja, ambayo ni jumla ya sh. milioni 43, ikiwa ni mchango wa bunge kwa familia kwa ajili ya matibabu

No comments:

Post a Comment