Tuesday, 7 March 2017
TUNDU LISSU AFUTIWA MASHITAKA NA KUKAMATWA NA POLISI
MBUNGE wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, jana, alikamatwa na polisi Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumfutia kesi ya jinai aliyokuwa akituhumiwa kutoa maneno ya kuwashawishi wananchi wa Zanzibar wasiridhike na wawe na nia ovu na serikali yao.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wa mahakama hiyo, alimfutia Lissu kesi hiyo na kumwachia huru, baada ya kukubaliana na hati iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ya kutokuwa na nia ya kuendelea kumshitaki mbunge huyo.
Ombi la kuondolewa kwa kesi hiyo mahakamani hapo, liliwasilishwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, ambaye aliieleza mahakama kwamba, DPP amewasilisha hati hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Lissu ambaye alikuwa akiwakilishwa na mawakili kadhaa, wakiwemo Peter Kibatala na Fredy Kiwelo, aliachiwa huru.
Hata hivyo, alipotoka tu katika chumba cha hakimu, alikamatwa na polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia.
Askari hao kutoka Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, waliondoka na mbunge huyo, ambaye alifika mahakamani hapo mapema asubuhi wakati shauri hilo lilipokuja kwa kutajwa hadi eneo la maegesho ya magari, ambapo walikuwa wameegesha gari lao.
Lissu, akiwa ameambatana na mawakili wake, aliwaeleza kuwa amefika mahakamani hapo akiwa anaendesha gari lake lenye namba za usajili T 216 DHH, aina ya Toyota Land Cruiser.
Kutokana na hilo, Lissu aliingia katika gari lake akiwa na askari na kuendesha hadi kituo cha polisi cha kati.
Akizungumza katika viunga vya mahakama, Wakili Kibatala alidai kwamba, hawajafahamu iwapo askari hao wamemchukua mbunge huyo kwa kuhojiwa kuhusu kesi hiyo au kama kuna nyingine.
Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alipandishwa mahakamani hapo Februari 8, mwaka huu na kusomewa mashitaka manne aliyokuwa akidaiwa kuyatenda Januari 11, mwaka huu, maeneo ya Kibunju Maungoni, Mjini Magharibi, Zanzibar katika kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Dimani.
Mbunge huyo alikuwa akidaiwa siku hiyo alitoa maneno ya ushawishi kwamba, tangu mwaka 1964, Tanganyika ndio inayoamua nani atawale Zanzibar.
Pia, alikuwa akidaiwa kutoa maneno yafuatayo: ‘Tangu mwaka 1964, Zanzibar inakaliwa kijeshi na Tanganyika, nani anayebisha? Tangu mwaka 1995, ikifika uchaguzi, askari wa Tanganyika wanahamia Zanzibar ili kuja kuhakikisha vibaraka wao wa Zanzibar, hawaondolewi madarakani na wananchi mnapigwa."
Aidha, anadaiwa alitamka: "Wananchi mnateswa, mnauawa kwa sababu ya ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar. Marehemu Karume alipoanza kushtuka mwaka 71 na 72, akauawa. Itakapofikia tarehe 15 mwezi wa kwanza, muadhimishe miaka 53 ya kukaliwa kijeshi na Tanganyika".
Maneno mengine aliyokuwa akidaiwa kuyatamka ni: ’ Jumbe aliondolewa Dodoma na Ally Hassan Mwinyi alipewa urais wa Zanzibar, Dodoma na aliyempa ni Nyerere, sio Wazanzibari. Marais wa Zanzibar wote ni made in Tanganyika. Wametengezwa na Tanganyika, wako madarakani kwa sababu ya Tanganyika."
Inadaiwa maneno hayo yalikuwa kwa ajili ya kushawishi watu wasiridhike na wawe na nia ovu. Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Lissu aliachiwa kwa dhamana kutokana na mahakama kukataa pingamizi la dhamana lililokuwa limewekwa na upande wa Jamhuri.
Hata hivyo, Lissu aliachiwa jana, jioni kwa dhamana na kutakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Machi 13, mwaka huu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment