Monday, 6 March 2017

JPM AMTUMBUA KIGOGO SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA


RAIS Dk. John  Magufuli amemtengua Mtendaji  Mkuu wa Shirika  Elimu Kibaha,  Dk. Crispin Mpemba  ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali za kiutendaji zinazomkabili.

Uamuzi wa kutenguliwa kwa kigogo huyo, umefikiwa kutokana na kuwepo kwa tuhuma za uendeshaji mbovu wa shirika hilo pamoja na mikataba yenye utata.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, alisema kutokana na kuwepo kwa tuhuma hizo, Rais Dk. Magufuli, amefikia uamuzi wa kutengua uteuzi wa mtendaji mkuu huyo, kuanzia Machi nne, mwaka huu.

“Ni kweli tuhuma kuhusu uendeshaji wa Shirika la Elimu Kibaha, ikiwemo suala la mikataba iliyoingiwa na shirika hilo ni za muda mrefu. Wizara hatukutaka kukurupuka kufanya uamuzi, hivyo tuliamua kuunda kikosi kazi kufanya uchunguzi na matokeo ya uchunguzi huo yalisababisha kuwepo kwa hoja zinazohitaji uchunguzi zaidi,” alisema.

Simbachawene alisema ili uchunguzi huo uweze kufanyika, Rais aliamua kumsimamisha kazi Dk. Mpemba, ili kupisha uchunguzi wa kina.

Alisema uamuzi wa kumsimamisha ulichukuliwa kwa sababu tuhuma za awali zilizojitokeza dhidi yake, zilijenga hoja ya kuhitajika kufanyika kwa uchunguzi zaidi.

Waziri huyo alieleza kuwa, kwa sasa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, inakaimiwa hadi uchunguzi utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment