Monday 6 March 2017

VIROBA VINGINE VYA BILIONI TANO VYANASWA DAR


OPERESHENI ya kusitisha uzalishaji, uuzaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya pombe kali kwenye vifungashio vya plastiki, maarufu viroba, imekamata shehena yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tano, katika maghala mawili, mali ya Lovekira  Enterprises, yaliyoko Kimara Temboni na Wazo Hill, Tegeta, Dar es Salaam.

Aidha, shehena hiyo, ambayo mmiliki wake ni  Elizabeth Masawe, ilikamatwa jana, jijini Dar es Salaam, katika msako mkali unaondelea.

Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kikosi cha Ubungo, John Nzila,  alisema katika ghala la Lovekira Enterprises, walikuta konyagii za mililita 100 katoni 14,393 na za mililita 50 zikiwa 9,964.

Aina nyingine ya pombe iliyopatikana katika ghala hilo ni Vradimil Vodca, mililita 50 katoni mbili, Zanzi mililita 90 katoni nane, Zanzi mililita 100 katoni 23, Value mililita 50 katoni 35 na Value mililita 100 katoni 233.

Nzira alisema wamesikitishwa na hatua ya wafanyabiashara hao kudharau agizo la serikali,  hivyo kuwataka wanaomiliki pombe hizo kujisalimisha kwa kuwa zoezi hilo ni endelevu.

"Hatutarudi nyuma katika kuwabaini wanaoendelea na biashara hii kwa kuwa mbali na serikali kusitisha kwa mujibu wa kanuni na sheria za vileo, bado wapo wanaokaidi,"alisema.

Alisema shehena hiyo ya viroba inaendelea kuhifadhiwa katika ghala la mmiliki kwa ajili ya hatua zaidi.

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Heche Suguta, alisema eneo la Wazo Hill Tegeta, wamevishikilia viroba vyenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni mbili, mali ya Lovekira  Enterprises.

Juzi, Waziri  Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba, alitangaza kuwa vita hiyo inaendelea huku kukiwa na katoni 99,171 ya pombe kali kwenye vifungashio vya plastiki yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 10.83, ambavyo vinashikiliwa na serikali.

No comments:

Post a Comment