ALIYEKUWA Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani na mwenzake, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Mwaifwani na aliyekuwa Kaimu Meneja wa Manunuzi wa MSD, Fredrick Nicolaus, walifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Vigogo hao wa MSD, walifikishwa mahakamani hapo mapema asubuhi kisha kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, ambapo Mawakili wa TAKUKURU, Leonard Swai na Aneth Mavika, waliwasomea shitaka moja la matumizi mabaya ya madaraka wakiwa na nyadhifa hizo.
Akiwasomea shitaka hilo, Wakili Aneth alidai washitakiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Alidai tarehe tofauti kati ya Machi Mosi na 19, mwaka 2013, katika makao makuu ya bohari hiyo, yaliyoko wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa nyadhifa zao, wakati wakitekeleza majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya.
Ilidaiwa washitakiwa hao walifanya hivyo wakati wa kuandaa na kutia saini mabadiliko ya mkataba namba moja wenye kumbukumbu namba MSD/003/Q/G/2010/2011/60 wa Machi mosi, 2013 na kuagiza kwa amri namba mbili yenye kumbukumbu namba MSD/003/Q/G/2010/2011/60 ya Machi 19, 2013.
Aneth alidai kitendo hicho kiliifanya H.H HILLAL & COMPANY LIMITED kupata manufaa ya sh.milioni 482, 266,000.
Washitakiwa hao, ambao wanatetewa na Wakili Gerald Nangi, walikana shitaka hilo, ambapo Wakili Swai alidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyingine kwa usikilizwaji wa awali.
Pia, upande huo wa Jamhuri, ulidai hauna pingamizi kuhusu dhamana kwa kuwa shitaka linalowakabili washitakiwa hao linadhaminika kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wa wakili wa washitakiwa, Nangi, aliiomba mahakama kutoa masharti nafuu kwa wateja wake.
Hakimu Mwijage alitoa masharti ya dhamana, ambayo yalimtaka kila mshitakiwa kuwa na mdhamini mmoja, atakayekuwa na barua ya utambulisho kutoka serikalini, shirika au taasisi yoyote iliyosajiliwa, ambaye atatia saini dhamana ya sh. milioni 20.
Masharti mengine ni kila mshitakiwa atadhaminiwa kwa kuweka mahakamani hapo hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya sh. milioni 200.
Washitakiwa hao waliweza kutimiza masharti hayo, hivyo waliachiwa kwa dhamana na kesi imepangwa kuanza kusikilizwa Machi 21, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment