Monday, 6 March 2017

APORWA BAJAJI NA KUUAWA KIKATILI


MKAZI wa Mtaa wa Mwayuge, Kata ya Igunga, wilayani Igunga mkoani Tabora,  Maduhu Dwisha (37), ameuawa kikatili baada ya kukodiwa na watu wasiojulikana kisha kumpora bajaji yake.

Mke wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la Mwadawa Jumanne (32), alisema jana kuwa, mume wake alitoweka nyumbani kwake Machi 2, mwaka huu, kuanzia saa nane mchana.

Alisema ilipofika saa mbili usiku, alianza kumtafuta kwenye simu, lakini hakuweza kupatikana.

Mwadawa alisema bila kukata tamaa, ilipofika saa tano usiku alipiga tena simu, ambapo alisikia sauti kwa mbali ikisikika kama mtu aliyetoka usingizini, hali iliyosababisha ashindwe kulala usingizi.

Alisema kesho yake alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Igunga, ambapo
polisi chini ya kiongozi wao ASP Paschal Kiula, waliondoka kwa kuungana na madereva wa bajaji zaidi ya 50 na kwenda hadi vijiji vya Igogo, Bulyang’ombe na Kata ya Nanga.

Aliongeza kuwa licha ya juhudi za kumtafuta marehemu katika milima ya maeneo hayo kwa saa nne, hawakufanikiwa kumpata, ndipo walipoamua kurudi mjini.

Kwa mujibu wa Mwadawa, wakiwa njiani afande huyo wa polisi alipigiwa simu kuwa, mwili wa marehemu umepatikana barabara ya Singida ukiwa umefichwa ndani ya daraja.

Alisema kwa kushirikiana na wananchi, waliutoa mwili wa marehemu katika daraja na kuupeleka hadi chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya huku simanzi na mayowe vikitawala.

Baadhi ya madiwani katika wilaya ya Igunga, akiwemo wa kata ya Igunga, Charles Bomani na wa viti maalumu, Teddy Patrick, Rukia Mwakibinga na Juliana Fabiano, walisema wana imani na polisi watafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kundi linalojihusisha na mauaji ya madereva wa bajaji mara kwa mara.

Kwa upande wao, baadhi ya waendesha bajaji ambao hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini, walisema polisi hawawezi kufanikisha kukomesha mauaji endapo wananchi, mafundi pikipiki na waendesha bajaji hawatatoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, kwa kuwa katika makundi hayo matatu, wapo wanaohusika na mauaji hayo.

Baada ya mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika hospitali ya wilaya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Igunga, Costa Olomi, aliitisha kikao cha dharura cha kamati ya siasa wilaya ili kujadiliana na serikali kuhusu suala zima la mauaji ya madereva wa bajaji.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Godfrey Mgongo, alikiri kupokea mwili wa  Maduhu Dwisha, ambapo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu aliuawa kwa kunyongwa shingo, ikiwa ni pamoja na kupigwa na kitu kizito usoni, hali iliyoachangia damu nyingi kuvuja kwenye ubongo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamisi Selemani Issa, alithibitisha kuuawa kwa mwendesha bajaji huyo na kusema kuwa, hadi sasa wanaendelea kuwasaka wahusika wa mauaji hayo, ikiwa pamoja na kuitafuta bajaji.

Alisema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo, polisi wataweka muda wa ukomo wa bajai kufanya safari za kubeba abiria nyakati za usiku na kuwataka waendesha bajaji kutokukubali kukodiwa usiku.

No comments:

Post a Comment