Monday, 6 March 2017

VIROBA VYA BILIONI 10.83 VYAKAMATWA DAR


OPERESHENI ya siku tatu ya kusitisha uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali za kwenye viroba, imewezesha kukamatwa kwa shehena ya katoni 99,171, yenye thamani ya zaidi ya  sh. bilioni 10.83.

Pia, imeibua wahamiaji haramu, nyaraka feki za serikali, kampuni zinazozalisha na kusafirisha pombe usiku na shehena ya viroba iliyokutwa imefichwa kwenye handaki maeneo ya Kariakoo.

Baadhi ya wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchambuzi wa kisheria wa madai yanayowakabili kukamilika huku wakionywa kuhusu shehena ya viroba iliyokamatwa na kudhibitiwa isiguswe wala kusafirishwa hadi taratabu za kisheria zitakapokamilika.

Aidha, kampuni tano zilizoweka zuio mahakamani kuhusu operesheni hiyo hazijafanikiwa.

Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, alisema kikosi kazi cha kitaifa cha serikali kinachotekeleza maagizo ya operesheni hiyo, kimefanikiwa kukamata shehena ya katoni 99,171, za viroba yenye thamani ya zaidi ya  sh. bilioni 10.83.

Makamba alisema wakaguzi 58, kutoka katika taasisi mbalimbali, ikiwemo jeshi la polisi, walihusishwa na kugawanywa katika timu tatu katika mikoa ya kikodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tutahakikisha tunasimamia viwanda, maduka, maghala na baa zinazofanya biashara kinyume cha sheria za udhibiti, ikiwemo ya chakula, dawa na vipodozi sura 219, sheria ya viwango namba 2 ya 2009, sheria ya vileo ya 1968 iliyorejewa 2012 na sheria ya usimamizi wa mazingira sura 191 na kanuni ya kukataza uzalishaji, uingizaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki,”alisema.

Alisema viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka 18, maghala manne, baa tatu, kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki, ikiwemo vifungashio, vimefikiwa ambapo viroba vya mililita 50, katoni 69,045 na mililita 100, katoni 29.344 za mililita 90, ni 782 na chupa za ujazo mililita 100 ni 10,625.

Makamba alisema chapa za pombe kali za viroba kama Red Wine, Banjuka, Officer’s Cane Sprit na Flash Ginna Dragon, hazikidhi viwango na hazijasajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) nchini.

Alisema kampuni zote zilizokamatwa hazina vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) na baadhi ya kampuni hazijalipa kodi na hazikuwa na cheti cha TFDA wala cheti cha TBS.

“Pia tumebaini kampuni mbili zilizokuwa zinazalisha na kusafirisha mzigo wa pombe usiku. Pia tumekamata viroba vyenye thamani ya sh. milioni 235, ambavyo vimekutwa vimefichwa kwenye ghala la duka la jumla chini ya jengo la ghorofa (handaki) maeneo ya Kariakoo,”alisema Makamba.

Aidha, alisema  baadhi ya pombe kali za aina mbalimbali zilikuwa zimefungashwa katika viroba na chupa, ambazo hazikuwa na namba ya toleo na tarehe za uzalishaji na nyingine hazikuwa na stika sahihi za TRA huku nyingine zikiwa na stika bandia.

Makamba alisema shehena hiyo ya viroba iliyokamatwa imezuiwa katika stoo za viwanda, maduka ya jumla, baa na maghala ya usambazaji na Idara ya Uhamiaji imeagizwa kushughulikia na kuwachukua hatua raia wa kigeni wasio na vibali vya kuishi nchini, ambao walikutwa kwenye baadhi ya viwanda.

Pia, aliagiza operesheni hiyo kuendelea nchi nzima kwa kasi zaidi kwa kuhusisha kamati za ulinzi na usalama na serikali za mitaa.

“Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kufungua kesi mahakamani dhidi ya wafanyabiashara waliokiuka katazo hili ili adhabu kali zitolewe na walioomba muda wa nyongeza kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, maombi hayo yatashughulikiwa baada ya oparesheni,”alisema.

Alisema kampuni tano zilizoweka zuio mahakamani hawakufanikiwa huku wafanyabiashara wanaolalamikia muda, wakitakiwa kutambua muda ulitolewa ni zaidi ya mwaka mmoja, hivyo kinachohitajika ni utekelezaji na wanaoamua kutotilia maanani agizo hilo la serikali kwa mazoea, hakutakuwa na huruma.

Katika kufanikisha oparesheni hiyo, serikali imetangaza zawadi ya sh. milioni moja kwa mtu atakayetoa taarifa itakayowezesha kushtakiwa na kukamatwa mtu anayezalisha, kuuza au kutumia stempu feki za TRA na sh. milioni moja kwa atakayewezesha kukamatwa na kushtakiwa mwenye kiwanda au mtambo wa kuzalisha viroba.

Pia, sh. 500,000 zitatolewa kwa taarifa za kukamatwa na kushtakiwa mwenye kuingiza nchini pombe za viroba na sh. 500,000 kwa atakayewezesha kushtakiwa na kukamatwa mwenye ghala au kuhifadhi shehena ya pombe hizo na sh. 500,000 kwa taarifa za anayesafirisha kinyume na sheria.

Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, alisema vipimo vilivyopo katika sampu ya awali ya pombe hiyo, imebaini sio  sahihi, lakini uwiano wa ujazo na plastiki zinazotumika vimetumika zaidi ya mara moja, hivyo vina matobo na uchakavu.

Naye Mkurugenzi wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema athari iliyopo katika pombe hizo ni pamoja na kiwango cha kemikali kinachosababisha madhara katika ini, hivyo kushindwa kufanya kazi na ongezeko la ajali za barabarani kwa watumiaji wa pombe hizo.

No comments:

Post a Comment