Monday, 6 March 2017
TUMEUDHIBITI MTANDAO WA DAWA ZA KULEVYA-SIYANGA
KAMISHNA wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Rogers Sianga, amesema wameshaudhibiti kwa kiasi kikubwa mtandao wa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Amesema wameshawakamata magwiji watano wa biashara hiyo, akiwemo mmoja, ambaye alikuwa anasambaza dawa hizo Tanzania Bara na Zanzibar.
"Kwa ujumla, idadi ya watu waliokamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya ni 11,000,"amesema Sianga.
Sianga alisema hayo jana, katika hafla ya Timu ya Taifa ya Vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys, ilipotembelea kituo cha vijana walioathirika na dawa za kulevya (sober house), kilichopo wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Alisema kwa sasa wanaendelea kupokea taarifa mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kutokomeza kabisa mtandao wa kuingiza dawa hizo hapa nchini.
Alisema wanatumia njia tatu katika kupata taarifa za watu wanaofanya biashara hiyo, ikiwa ni pamoja na taarifa za watu za moja kwa moja, utafiti na wananchi.
Hata hivyo, Sianga amekiri kuwa vita ya kupambana na dawa za kulevya ni kubwa kutokana na kila siku wahusika wanabuni njia mpya.
Alisema vita hiyo sio lelema kutokana na ukweli kuwa, wanaofanya biashara hiyo wana mbinu nyingi za kufanya kila kukicha.
Hata hivyo, Sianga amesema wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa, wahusika wote watakamatwa na kusisitiza kuwa, hawataingia kichwa kichwa katika kufanya kazi hiyo.
Sianga alisema anajisikia furaha kuona kuwa, viongozi wa dini wako mstari wa mbele katika vita hiyo na kumfanya atembee kifua mbele.
Alisema watashirikiana na watu wa 'sober house' katika kutoa mihadhara ya kuelimisha jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya kwa wale waliotumia na ambao kwa sasa wamepona.
Mkurugezi wa Sober House, Al-Karim Banji, alisema kuwa changamoto iliyokuwa mbele yake katika kituo hicho ni kukosa eneo, ambalo linaweza kukidhi mahitaji kwa wanaume na wanawake.
Alisema kwa sasa kituo hicho kinapokea wanaume pekee, wakati wapo wanawake walioathirika, lakini hawajaweza kupata msaada huo.
Kamishina huyo alitoa msaada wa kompyuta moja kwa ajili ya kuendesha kazi za kituo hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Hassanoo alitoa hekari moja wakati Rais wa TFF, Jamal Malizi alitoa fedha taslimu sh. milioni 1.2, mipira na jezi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment