Monday, 6 March 2017

JPM: NITAENDELEA KUWATUMBUA MAFISADI SERIKALINI

RAIS Dk. John Pombe Maghufuli amezisizitiza kuendelea na vita ya kupambana na ufisadi kwa kuwaondoa mafisadi serikalini na kuwafikisha mahakamani ili kuokoa fedha za umma ziweze kufanya kazi za maendeleo ya wananchi.

Akiwahutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Mtwara na vitongoji vyake, waliofurika katika Uwanja wa Mashujaa, mjini hapa jana, Rais Magufuli alisema wanaopinga utumbuaji wa majipu ndiyo mafisadi wenyewe.

Alisema kumekuweko na ufisadi wa njia mbalimbali, ambao ulikuwa unapoteza mamilioni ya fedha za serikali kwa kulipia huduma na wafanyakazi hewa.

Alitoa mfano wa kubainika kwa watumishi hewa takribani 19,000, waliokuwa walipwa mishahara na posho na wanafunzi hewa 56 000, ambapo kugundulika kwao kuliwezesha mamilioni ya fedha za serikali kuokolewa.

"Ninawashukuru kwa wanaotupongeza kwa kutumbua majipu, wanaopinga ni mafisadi wenyewe hao, hata hapa yapo na tutayatumbua," alisema Rais Magufuli huku akishagaliwa kwa nguvu na kuwauliza wananchi iwapo aache kuwatumbua, ambapo alijibiwa kwa sauti za juu kwamba aendelee.

Aliwataka wananchi wakatae kutumika na wanasiasa uchwara, ambao siku zote kazi yao ni kuichonganisha serikali na wananchi.

Rais Magufuli alielezea kazi, ambazo serikali yake imezifanya katika kusukuma maendeleo ya taifa tangu aingie madarakani mwaka 2015.

Alisema aliweka kipaumbele katika maendeleo ya elimu, hasa katika kuhakikisha watoto wa wananchi masikini wanapata haki hiyo ya kupata elimu bora na siyo bora elimu.

Rais Magufuli alisema alianza na kutoa jumla ya sh. billioni saba kila mwezi za ada na mahitaji mengine muhimu katika shule za msingi na sekondari, ili kuwezesha wanafunzi kusoma bila kubughudhiwa na michango mbalimbali.

"Hatua hii imeondoa kufukuzana fukuzana, sasa hakuna anayefukuzwa shuleni," alisema Rais Magufuli na kueleza kuwa, hatua hiyo imeongeza idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa darasa la kwanza takbriban kwa asilimia mia moja.

Alisema ongezeko hilo pia lipo kwa shule za sekondari kwa asilimia 27, huku mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu ikiongezeka.

Rais Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na kushuka kwa kiwango cha elimu mkoani Mtwara, ambako miaka ya nyuma ulikuwa unafanya
vizuri na kutoa viongozi wengi wa nchi.

"Haiwezekani serikali tunaupeleka mkoa kuwa kitovu cha maendeleo, ninyi wenyewe mnaupeleka kuwa kitovu cha wajinga," alisema Rais Magufuli kuonyesha kusikitishwa na matokeo hayo mabaya.

Alitoa wito kwa wadau wote wa elimu mkoani hapa, kukaa pamoja na kuja na uamuzi wa hatua za kuchukuwa ili kuukwamua katika maendeleo
duni ya elimu.

Alihimiza zaidi wananchi kufanyakazi kwa bidii ili kunufaika na kursa za uwekezaji na miradi mikubwa, miundombinu ya kiuchumi na maendeleo, inayojengwa mkoani hapa.

Alisema wananchi watimize wajibu wao na serikali nayo itatimiza wajibu wake wa kuwaletea maendeleo Mtwara.

Katika hutoba hiyo, pia alikemea makato ya hovyo kwa wakulima wa
korosho  na kuagiza kuchukuliwa hatua vyama vya ushirika vinavyowaibia wakulima kwa njia hiyo, kikiwemo cha Masasi.

Awali, Rais Magufuli alifungua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la viwandani mjini hapa na ujenzi wa njia ya msongo wa kusambazia umeme
kwa mkoa wa Lindi wa kilowatt 132.

Mbali na kuipongeza TANESCO kwa kazi nzuri, pia aliitaka kukusanya madeni yake kwa kasi bila kujali mtu.

No comments:

Post a Comment