Monday, 6 March 2017

UTAFUTAJI MAFUTA NA GESI ZANZIBAR KUANZA KARIBUNI


HATIMAYE kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar, itaanza wakati wowote kuanzia sasa, kwa kutumia ndege maalumu, ikijumuisha maeneo yote ya nchi kavu na baharini katika visiwa vikubwa na vidogo.

Akitoa taarifa ya serikali kuhusu kuanza kwa kazi hiyo, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Aboud Talib, alisema jana, kwamba kazi ya awali ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia itaanza kwa kitalu cha Pemba.

“Nawajulisha wananchi wote wa Unguja na Pemba kuwa, hivi karibuni kazi ya awali ya  utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia itaanza katika kitalu cha Pemba - Zanzibar, kinachojumuisha maeneo yote ya nchi kavu ya visiwa vyetu vikubwa na vidogo na maeneo ya bahari iliyozunguka visiwa hivyo,”alisema waziri huyo.

Waziri Salama alisema kazi hiyo itafanywa na Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, ikitumia ndege kukagua miamba iliyoko chini ya ardhi, ambapo kwa kitaalamu kazi inajulikana 'Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey (FTG)'.

“Ndege hii itaruka karibu na mgongo wa dunia kwa wastani wa mita 80, kutoka usawa wa bahari kwa maeneo ya nchi kavu na wastani wa mita 120 kutoka usawa wa bahari kwa maeneo ya baharini,” alisema Waziri Salama katika taarifa yake hiyo.

Aliongeza kuwa, kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa kitalu cha Pemba- Zanzibar, itachukua miezi minne, ambapo serikali inawaomba wananchi wasiwe na hofu wakati kazi hiyo ikiwa inaendelea kwa kuwa hakutakuwa na athari yoyote itakayotokana na shughuli hiyo.

Aidha, alisema serikali inawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu watakaoshiriki katika kazi hiyo ili iweze kufanyika kwa wepesi na kwa kiwango kinachotakiwa.

“Ni dhahiri kuwa wananchi wa Zanzibar wamekuwa na shauku ya muda mrefu kutaka Zanzibar ianze kutafuta na hatimaye kuchimba rasilimali ya mafuta na gesi asilia. Sote tunaamini rasilimali hii itasaidia kukuza uchumi wetu,”alisema waziri huyo.

Kuanza kwa kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, kunaanza baada ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein kutia saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, Novemba, mwaka jana.

Waziri Salama alisema kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo, Serikali ilitengeneza Sera ya Mafuta na Gesi Asilia kwa ajili ya kutoa muongozo kwa sekta hii muhimu katika uchumi wa nchi.

Kutungwa kwa sheria hiyo kunatokana na masharti ya kifungu cha nne Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia 2015 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inataja kwamba, shughuli za uendeshaji wa mafuta na gesi asilia utafanywa Zanzibar kwa kusimamiwa na kuendeshwa na taasisi kwa mujibu wa Sheria za Zanzibar.

Kwa mara ya kwanza kabisa, kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ulifanyika Zanzibar mwaka 1952, ambapo utafiti huo ulionyesha kuwepo kwa dalili za mafuta katika maeneo ya Pemba na Unguja.

No comments:

Post a Comment