Monday 6 March 2017

JPM AAGIZA DANGOTE APEWE KITALU CHA MAKAA YA MAWE


RAIS Dk. John Magufuli ameagiza Kiwanda cha Saruji cha Dangote kupewa kitalu cha kuchimba makaa ya mawe kwa matumizi ya kiwanda, badala ya kuuziwa na mwekezaji mwingine aliyepewa mgodi huo.

Sambamba na agizo hilo, pia ametaka Dangote apewe maeneo ya kuchimba malighafi na kuuziwa gesi moja kwa moja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), badala ya kutumia kampuni ya kati (madalali).

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipotembelea kiwanda hicho kikubwa cha kisasa cha saruji katika ukanda wa kati na kusini mwa Afrika, kilichojengwa katika Kijiji cha Msijute, nje kidogo ya mji wa Mtwara, ambapo alizindua rasmi magari 580, ya usambazaji wa saruji nchi nzima.

Rais Magufuli alitoa siku saba kwa Wizara ya Nishati na Madini na TPDC, kuhakikisha inatoa leseni kwa kiwanda hicho ya kuchimba makaa wa mawe.

Kiwanda cha Dangote kilichoanza  uzalishaji mwaka mmoja uliyopita, kilikumbana na changamoto nyingi, zikiwemo upatikanaji wa nishati ya kuendeshea mitambo yake na kusababisha kusimamisha uzalishaji.

Rais Magufuli alisema alitaka kuitumia siku ya jana, kumaliza matatizo na  mizengwe iliyojitokeza na kuathiri uzalishaji, ikiwemo upatikanaji wa makaa ya mawe.

Alisema nchi inayo makaa ya mawe ya  kutosha, lakini yamemilikishwa kampuni moja isiyo na uwezo na kusababisha urasimu wa upatikanaji, jambo ambalo linaweza pia kuongeza gharama za uzalishaji na kupandisha bei ya saruji.

"Ugonjwa huu ninataka kuumaliza leo,"alisema Rais Dk. Magufuli na kuongeza kuwa, inawezekana kuna watu wanahujumu kiwanda hicho kwa sababu ya wivu wa kibiashara, hasa wenzake wa sekta hiyo ama wapo watu hawataki Mtwara iendelee.

"Sasa ninaagiza mkatieni Dangote kipande cha mgodi huo achimbe mwenyewe, nataoa siku saba awe amekabidhiwa leseni," aliagiza Raisi huku akishangiliwa kwa nguvu na umati mkubwa wa watu  uliohudhuria hafla hiyo.

Umati huo kutoka vijijini na mjini Mtwara, awali ulizuiwa kuingia kiwandani hapo,  lakini Rais Dk. Magufuli alisimamisha msafara wake wakati wa kuingia na kuamuru watu wa usalama kuwaingiza kwanza wananchi hao.

Alisema amekuwa akiambiwa matatizo mengi ya kiwanda hicho, ikiwemo magari hayo kukaa bandarini kwa takribani miezi miwili bila kutolewa kwa sababu mbalimbali.

Lakini cha ajabu, alisema alipopiga simu kuuliza kuna nini hapo bandarini, malori hayo  yaliondolewa mara moja.

Rais Dk. Magufuli alisema kampuni iliyowekeza katika mgodi wa makaa ya mawe haina uwezo mkubwa wa kutosheleza mahitaji ya makaa ya kiwanda cha Dangote.

Alisema ufumbuzi pekee ni wao wenyewe, Dangote kupewa eneo la kuchimba, hata kama mengine atauza nje, mradi afuate taratibu na sheria na likiisha wamkatie lingine.

Rais alisema ameshangazwa na taarifa kuwa, hata gesi ya TPDC nayo Dangote alipangiwa kuuziwa kupitia kampuni nyingine ya kati (madalali), inayodaiwa kuanzishwa na baadhi ya watendaji wa kiwanda hicho.

Aliagiza TPDC kujenga bomba la kufikisha gesi kiwandani hapo moja kwa moja kutoka shirika hilo, badala ya kutumia mtu wa kati.

"Inashangaza sana kuona mmejenga bomba la gesi kutoka Madimba mpaka Kinyerezi, Dar es Salaam, lakini mmeshindwa bomba la kilomita kumi la kuingiza kiwandani,"alisema.

Rais Magufuli alimwambia Alhaji Aliko Dangote kuwa, matatizo mengine yapo ndani ya menejimenti ya kiwanda chake, ambayo yanakwamisha na kuathiri uzalishaji kwa sababu zao binafsi.

Alitoa mfano wa urasimu wa uajiri wa madereva wa magari hayo kuwa, unatokana na menejimenti hiyo kuwapa madalali wa ajira, ambao wanadaiwa kutoa ajira kwa urasimu mkubwa wenye harufu ya rushwa.

Kuthibitisha hilo, alimwita mmoja wa waomba kazi ya udereva, ambaye kwa niaba ya wenzake, walitoa malalamiko yao na tuhuma kwa uongozi wa kiwanda katika kutoa ajira hizo.

Mapema, Dangote alitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kuajiri wafanyakazi 20,000 wa moja kwa moja na kupitia kampuni zinazotoa huduma kiwandani.

Alisema malori hayo yataajiri watu 1,500 na yatasambaza saruji hadi vijijini nchi nzima, kwa bei nafuu isiyozidi sh. 10,000, ili kuwawezesha wananchi kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora.

Dangote alisema uzalishaji kwa sasa ni tani 500,000 hadi 770,000, kwa mwaka na mwaka huu, wanatarajia kuzalisha tani milioni mbili na mwakani kufikia lengo la tani milioni tatu.

Alisema mradi huo mkubwa wa uwekezaji uligharimu Dola za Marekani milioni  630, pia utawanufaisha wananchi wa vijiji jirani kwa kujenga huduma za kijamii za maji, hospitali na soko kubwa la biashara.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli jana, alizindua kituo cha kupooza umeme cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kilichoko mjini Mtwara, ambacho kinajengwa na wataalamu wa TANESCO, kwa gharama ya sh. bilioni 16, mradi ambao utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 132, kutoka Mtwara hadi Lindi, hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Lindi.

Rais Magufuli alimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na menejimenti na wafanyakazi wa TANESCO, kwa kazi nzuri wanayofanya, iliyowezesha usambazaji wa umeme kuongezeka hadi kufikia asilimia 46, nchi nzima, lakini alitoa maagizo kwa TANESCO, kuwakatia umeme wote wenye madeni bila kujali kama ni taasisi ya umma ama binafsi.

Mapema jana asubuhi, Rais Dk. Magufuli alisali ibada ya Diminika ya Kwanza ya Kwaresma, katika Kanisa la Watakatifu Wote, Jimbo Katoliki la Mtwara, ambako alichangia sh. milioni moja na mifuko 200, ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa kanisa na ukarabati wa kanisa na kuwataka wananchi wa Mtwara, kushikamana kuiombea nchi na kufanyakazi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na taifa zima.

No comments:

Post a Comment