Sunday 5 March 2017

VUAI: MATATIZO NDANI YA CCM YATATULIWE KWA KANUNI, KATIBA


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,  Vuai Ali Vuai, ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Mjini kichama, kufuatilia sababu za kufukuzwa kwa viongozi wawili wa Jimbo la Jang’ombe na kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo haraka kupitia miongozo na kanuni za Katiba ya Chama.

Amesema CCM ina utaratibu wa kushughulikia migogoro ndani ya Chama na Jumuia zake katika ngazi mbalimbali, kwa kufuata misingi ya Katiba, hivyo  lazima kasoro zinazojitokeza ndani ya taasisi hiyo zitatuliwe kwa utaratibu uliowekwa, badala ya matakwa binafsi ya baadhi ya viongozi.

Vuai amesema kwa mujibu wa kanuni za masuala ya uongozi, kamati za siasa za majimbo, hazina mamlaka ya kuwafukuza ama kuwaondosha katika nafasi za uongozi watendaji wa ngazi za majimbo, badala yake wanatakiwa kufanya vikao vya kikatiba kuwajadili watuhumiwa na kuwasilisha mapendekezo yao kwa ngazi ya wilaya ili  kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia taratibu za CCM.

Alitoa agizo hilo jana, kutokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa viongozi wawili waliovuliwa nafasi za uongozi katika jimbo hilo.

Viongozi hao walimweleza Vuai kuwa, wameonewa kwani wamefukuzwa wakiwa hawajui kosa linalowakabili na bila kupewa nafasi za kujieleza.

Vuai aliutaka uongozi wa wilaya hiyo, kufuatilia kwa kina mgogoro huo ili umalizike bila kuathiri uongozi wa jimbo hilo, na kuwasihi viongozi, watendaji na wanachama, kusoma Katiba ya CCM na kanuni zake kwa lengo la kujikumbusha mambo ya msingi yatakayosaidia kuepuka kasoro zisizokuwa za lazima.

“Chama Cha Mapinduzi kinaongozwa kwa misingi ya kikatiba na maamuzi mbalimbali yanayofanyika, yanafuata muongozo huo na kila ngazi imepewa majukumu yake kulingana na kanuni zetu, hivyo nakukumbusheni kuwa viongozi tuwe makini kuhakikisha tunasoma kwa makini katiba na kanuni zinazotuongoza," alisisitiza.

"Lakini tusikubali kugawanyika kwa tofauti ndogo ndogo zinazojitokeza kama changamoto ndani ya Chama chetu na tunaposhutumiana hadharani,  tunavunja utaratibu unaotuongoza ndani ya taasisi yetu”, alisema Vuai na kusisitiza kuwa, umoja, upendo na ushirikiano ndani ya jimbo hilo na CCM kwa ujumla ndio siri ya mafanikio.

Aliwaambia wanachama hao kuwa, mabadiliko ya kimuundo yanayofanyika ndani ya taasisi hiyo, yanalenga kujenga Chama chenye nguvu za kiuchumi, utakaotokana na matumizi mazuri ya rasilimali zake kwa maslahi ya wanachama wote.

Kupitia ziara hiyo, aliwakumbusha viongozi na watendaji wa CCM, kusimamia vizuri miradi ya Chama ili isaidie shughuli za kiutendaji na kuwanufaisha wanachama wote, badala ya watu wachache.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini, Juma Fakih Choum, alimueleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa, baada ya kupata malalamiko ya kufukuzwa kwa viongozi hao, wilaya ilichukua hatua za kuuagiza uongozi wa jimbo, kukutana pamoja katika kikao ili wajadiliane na kutafuta ufumbuzi wa kumaliza mzozo huo.

No comments:

Post a Comment