SIKU chache baada ya mfanyabiashara Mohamed Ikbal, kudaiwa kumpa hekari 1,500 zenye mgogoro, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mfanyabiashara huyo ameibuka na kutoa ufafanuzi juu ya sakata hilo na kusisitiza kwamba eneo hilo anamiliki kihalali.
Ikbal, ameibuka wiki chache baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kueleza kuwa eneo hilo lililoko Lingato, Kisarawe II , Kigamboni jijini Dar es Salaam, ni mali ya serikali baada ya mfanyabiashara huyo kushindwa kesi dhidi ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mjini Dar es Salaam, kwa niaba ya mfanyabiashara huyo, Kamugisha Katabaro, alisema Ikbal anamiliki hekari 3,500, katika eneo hilo la Lingato, Kisarawe II, tangu mwaka 2005.
Alisema Ikbal alinunua eneo hilo kutoka kwa wananchi, ambao waliuza kwa hiyari yao wenyewe bila kushurutishwa na kwa kufuata taratibu zote za kisheria.
“Ushahidi wa nakala za barua za mawasiliano kati ya serikali ya mtaa wa Lingato, muhtasari wa vikao vya maamuzi ya serikali ya mtaa na mikutano ya wananchi waliokuwa wamiliki maeneo hayo ipo,”alisema Katabaro.
Aliongeza: “Nakala za stakabadhi za malipo ya ushuru wa serikali ya mtaa kama sheria inavyotaka, mikataba ya mauziano ya maeneo ya ardhi, sambamba na picha za wamiliki wa maeneo wakipokea fedha za malipo ya mauziano ya ardhi zipo na zitawekwa bayana zikihitajika.”
KUZUKA KWA MGOGORO
Katabaro alisema miaka michache baada ya mauziano hayo, baadhi ya wananchi waliingwa na tamaa kutokana na kupanda kwa thamani ya ardhi.
“Kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa wasio waaminifu, walianza kuvamia eneo hilo na baadaye kuwasilisha malalamiko kwa Kamishna wa Ardhi kwamba wananyanyaswa katika ardhi yao na kwamba, hawakuuza maeneo hayo kwa hiari yao,”alisema Katabro.
Alisema Ofisi ya Ardhi katika barua yake ya Oktoba 31, 2006, yenye Kumbukumbu Na. LD/164035/CB, iliuomba uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, kutoa taarifa juu ya malamiko ya kundi hilo.
“Katika barua yenye kumbukumbu Na. TMC/MD/M.13/83/79 ya Desemba 18, 2006, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke alimjulisha Kamishna wa Ardhi kuwa, mgogoro huo ulishughulikiwa na Kamati ya Rais ya Kushughulikia Migogoro chini ya Mstahiki Meya wa manispaa hiyo," alibainisha Katabaro.
Aliendelea kueleza kwamba, kufuatia majibu hayo, Kamishna wa Ardhi alilitaarifu kundi hilo la walalamikaji kupitia barua yenye Kumb. Na. LD/164035/VOL.V/39 ya Februari 26,2007.
“Licha ya majibu ya Kamishna wa Ardhi, bado mgogoro huo uliendelea na kumfanya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, kufanya mkutano kati ya wananchi na Ikbal, uliofanyika Oktoba 8, 2007, ambao ulianyika katika eneo la Asha Ngoma, Kisarawe II ,”alisema.
Aliongeza: “Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, alihitimisha mkutano huo kwa kuwataka wale wote, ambao wanahisi kudhulumiwa kupeleka malalamiko yao mahakamani.”
Katabaro alisema kutokana na kuendelea kwa uvamizi katika eneo hilo, Ikbal aliwasilisha malalamiko yake katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, ambaye alimuandikia barua Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi ya Kigamboni, kupitia barua ya Februari 26, 2008, yenye kumbukumbu Na. E.40/9/VOL.1/64, kumjulisha juu ya malalamiko hayo na kumtaka kuchukua hatua.
“Kundi la pili la wavamizi liliwasilisha malalamiko yao kwenye Ofisi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupitia barua ya Machi 4, 2008,”alibainisha Katabaro.
Aliongeza kuwa baada ya kufuatilia kwa kina, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, iliwajibu kwa barua ya Mei 9, 2008 yenye kumbukumbu Na. EA71/176/01.B/49, ikibainisha kwamba wananchi hao waliuza maeneo yao kwa hiari.
KUMKABIDHI ENEO MAKONDA
Katabaro alisema mchakato wa kulipitia eneo hilo ili kukamilisha mchakato wa kulikabidhi kwa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, ulizingatia taratibu zote.
“Ikbal aliamua kutoa ene hilo kwa mkoa wa Dar es Salaam, kwa hiari ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza viwanda,”alieleza.
Alisema hakuna utata wowote katika eneo hilo kwani taratibu za kumkabidhi Makonda zilifuatwa.
Katabaro alisema Ikbal ameamua kutoa maelezo hayo sio kwa kumjibu Waziri Lukuvi, bali kuweka ukweli wa mambo ili jamii iweze kuufahamu.
No comments:
Post a Comment