Sunday 5 March 2017

SERIKALI SASA YAAGIZA POMBE KALI ZIWEKWE KWENYE CHUPA


KATIKA kukabiliana na matumizi ya pombe maarufu ya viroba, serikali imeziagiza kampuni zinazozalisha pombe kali, kubadilisha teknolojia ya ufungaji wake na kuweka vinywaji hivyo kwenye chupa kutoka katika viroba.

Pia, imeeleza namna ambavyo Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, inaendelea na utendaji wake wa kazi, ambapo imekamata na kuwatia hatiani watuhumiwa 76, waliokutwa dawa za viwandani, ambazo ni heroine na cocaine.

Agizo hilo lilitolewa jana mjini hapa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akifungua kikao cha baraza la mawaziri, ambacho ni cha kwanza kufanyika mkoani Dodoma, baada ya serikali kuhamia Dodoma.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine, moja ya ajenda yake ni mawaziri ambao ni wajumbe wa tume hiyo, kupokea taarifa ya kazi iliyokwishafanywa katika kukabiliana na dawa za kulevya tangu kuanza kazi kwa tume hiyo.

Agenda nyingine ni kila wizara kutoa taarifa na idadi ya watumishi waliohamia Dodoma, kwa awamu ya kwanza na kueleza mpango waliojiwekea katika kukamilisha kuhamia Dodoma na katika awamu ngapi kati ya awamu sita zilizopangwa.

“Baada ya taarifa, watapata maelekezo kidogo kwenye agenda hiyo, lakini pia ningependa kujua kwa sasa ofisi zenu zipo wapi, kwa sababu baadae waziri mkuu nitafanya ziara kuona shughuli zinazoendelea na kuona kazi ya utoaji huduma ili kujiridhisha Watanzania kwamba, azma yetu ya serikali kuhamia Dodoma imekamilika,”alisema.

Aliitaja nyingine kuwa ni kupokea taarifa ya matumizi ya fedha na miradi ya maendeleo kwa Julai 2016 hadi Februari 2017, agenda ambayo haitajadiliwa kama mwanzo kwa kila wizara kutoa taarifa ya fedha iliyoingia na kazi zilizofanywa, badala yake watapata taarifa kutoka kwa Waziri wa Fedha.

VITA ZA DAWA ZA KULEVYA

Akitoa taarifa ya mwenendo wa vita dhidi ya dawa za kulevya, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Tume hiyo ilianza kazi Februari, mwaka jana na katika kipindi cha Julai 2016 hadi Januari 2017, watuhumiwa 11,503, wamekamatwa kwa kujihusisha na uzalishaji, uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa hizo.

Majaliwa alibainisha kuwa, kati ya watuhumiwa hao,  9, 811 walikutwa na kesi za kujibu huku 974, wakitiwa hatiani baada ya kubainika kuhusika na makosa hayo.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaagiza mawaziri wote, ambao ni wajumbe wa tume ya kuratibu udhibiti wa dawa ya kulevya nchini, kushiriki kikamilifu katika vita hiyo huku akiwakabidhi namba ya kamishina wa dawa za kulevya ili waweze kumpatia taarifa mara wanapokutana na matukio yanayohusiana na dawa za kulevya.

Kuhusu pombe haramu na pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki, maarufu kama viroba, Waziri Mkuu Majaliwa alisema msako wa kuondoa bidhaa hizo, ambazo zilikuwa zikihatarisha ustawi wa taifa unaendelea.

Alisema katika msako huo, walibaini kuwepo kwa kwa kampuni zinazozalisha pombe hizo bila vibali huku wengine wakiweka pombe haramu ya gongo kwenye viroba hivyo.

“Katika vita hivi mambo mengi yataibuka maana hivi sasa tumebaini hayo.
Tunaamini tunapoendelea na msako, tutabaini mambo mengi makubwa zaidi na pia kutokuwa na vibali kumesababisha wafanyabiashara hao kukwepa kulipa kodi,”alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kukamilika kwa mawaziri wote kuhamia Dodoma, huku akiwataka kufanyia shughuli zao zote mkoani humo.

“Dodoma ndio makao makuu, hivyo hapa ndio tumefika, Dar es Salaam tutaendelea kuiboresha ili ibaki kuwa mji wa biashara kama tulivyopanga na Arusha, yote itakuwa miji ya biashara,”alisisitiza Majaliwa.

No comments:

Post a Comment