Sunday, 5 March 2017

JPM AAMURU HATI YA KUSAFIRIA YA MKANDARASI ISHIKILIWE HADI AMALIZE MRADI WA MAJI

RAIS Dk. John Magufuli ameagiza kushikiliwa hati ya kusafiria ya mkandarasi wa Kampuni ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India, Rajendra Kumar na wasaidizi wake, mpaka atakapokamilisha mradi wa maji wa Ng'apa mjini Lindi.

Pia, ametoa miezi minne kwa mkandarasi huyo kumaliza kazi, ambayo ilipaswa kukamilika Machi, 2015 na kumtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, kuunda timu ya watu watakaomsimamia mkandarasi huyo.

Alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Ilulu, Lindi, baada ya kufanya ziara kwenye mradi huo, ambao alizuiwa na Waziri wa Maji kuutembelea.

Katika mradi huo, alisema alikuta hakuna kilichofanyika licha ya kutumia miaka sita kujengwa, lakini hadi sasa haujakamilika na ulitarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni tano za maji kwa siku, kwa ajili ya wakazi wa Lindi, ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.

Alisema mradi huo anaujua kwa kuwa siku ya kuwekwa jiwe la msingi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alishiriki akiwa Waziri wa Ujenzi.

"Najua Waziri Injinia Gerson Lwenge (Waziri wa Maji na Umwagiliaji), aliniambia nisiende kwenye mradi kwa kuwa hakuna kilichofanyika na mimi nikamwambia hapana, ngoja niende na nimeshuhudia,''alisema.

Alisema aliamua kuchukua maamuzi dhidi ya mkandarasi huyo, lakini amekubali ushauri aliopewa na waziri wa kuhakikisha ndani ya miezi minne, mradi huo ukamilike na usipokamilika. atachukua hatua ambazo kila mtu atalalamika.

Dk. Magufuli alieleza kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo, ambao tayari kiasi cha sh. bilioni 21.8, zimetolewa kati ya sh. bilioni 29, zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake.

"Ikipita miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wana shida ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India, mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo la ujenzi, halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" Alihoji Rais Magufuli.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, kuchukua hati ya kusafiria ya mkandarasi huyo na kuhakikisha katika kipindi chote cha miezi minne ya ujenzi wa mradi huo, haondoki kwenye eneo hilo hadi mradi utakapokamilika.
    
Rais Dk. Magufuli alisema kama tatizo ni fedha ndio sababu mradi haumaliziki, aambiwe ili atoe fedha serikali kuu iweze kuukamilisha wananchi waweze kupata maji safi na salama.

Kuhusu ombi la Nape Nnauye, alilolitoa awali juu ya kuongezeka kwa bei ya korosho, Rais Magufuli alisema kuongezeka kwa bei kunatokana na mambo kadhaa, ikiwemo ubora wa bidhaa na kufanyakazi.

Alisema uzalishaji unapaswa kuendelea kukua, hivyo wana Lindi, hususan vijana, wanatakiwa kufanya kazi mashambani ili kuepuka kufa na njaa wakati wanazo fursa likuki kwenye mkoa wao.

"Naomba niseme ukweli, mimi sio mwanasiasa wa kutumia uongo kupendwa na watu na niwatake wanasiasa, waelezeni wananchi ukweli. Bila kufanya kazi mtu utakufa na njaa, niko tayari kuchukiwa na mtu, lakini niseme ukweli kwa sababu serikali hailimi korosho bali wananchi.

"Ninawapongeza sana wana Lindi kwa kazi nzuri mliyoifanya kulima vizuri korosho msimu uliopita, jambo lililofanya mkauza vizuri na kupandisha bei ya korosho. Nawaambia itaendelea kupanda kwa sababu serikali iko pamoja na ninyi," alisema.

Aliongeza pia kuwa, Lindi ni eneo zuri kwa viwanda, ambapo kwa sababu serikali yake ni ya uchumi wa viwanda, kutaanzishwa kiwanda kikubwa cha mbolea katika mkoa huo, ambacho kitatoa ajira za watu zaidi ya 10,000.

"Viwanda hapa Lindi lazima vije, mnavyo viwanda vidogo vingi vya chumvi, mnaweza kuvifanya vikawa vikubwa tu, lakini niwaambie uongozi wa mkoa huu, wawekezaji hawaji hivi hivi, tengenezeni mazingira ya kuvutia wawekezaji," alisema Rais.

Aidha, alisema kuhusu tabia ya viongozi wa vyama vya msingi kuwaibia wananchi, uongozi wa mkoa unatakiwa kushughulika nao kwa kuwasaka na kuwapeleka kwenye mkono wa dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Kuhusu ahadi yake ya kivuko aliyoitoa kipindi cha kampeni zake za urais, Rais Magufuli alisema ataleta kivuko hicho hata kama ni kukitoa Dar es Salaam, ambako tayari kuna Daraja la Nyerere, lililoko Kigamboni.

Alitumia fursa hiyo kuwasifu wateuzi wake kutoka mkoa wa Lindi, akiwemo Waziri Nape Nnauye (Mbunge wa Mtama), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mama Salma Kikwete, ambaye alitaja sababu za kumteua.

Dk. Magufuli alisema aliamua kumteua Mama Salama Kikwete kuwa mbunge kwa kuwa ni mchapakazi na anakipenda Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Mama Salma ni mchapakazi kwelikweli, na mbali ya uchapakazi, pia ni mzuri. Naamini shida nyingi mtafikisha kwake," alisema na kushangiliwa na mamia ya wananchi uwanjani hapo.

Kwa upande wake, Salma Kikwete, ambaye ni mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alisema anashukuru uteuzi alioupata wa Rais Dk. Magufuli kwa kuwa anaamini atafanya kazi kwa bidii kubwa.

"Rais Magufuli nakushuru sana kwa kuniteua kuwa mbunge, mimi pamoja na wana Lindi tunakuunga mkono kwa kazi kubwa unayoifanya,'' alisema.

Alisema uteuzi huo ameupokea kwa mikono miwili na anaahidi atafanya kazi kwa bidii kubwa kwa ajili ya maslahi ya watu wa Lindi na Taifa kwa ujumla.

Rais Magufuli anatarajiwa kukamilisha ziara yake mkoani Lindi na baadaye ataanza safari ya kwenda mkoani Mtwara, atapofanya ziara yake leo na kesho.

Katika kuhitimisha ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, Rais Magufuli atahutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.

No comments:

Post a Comment