Friday, 3 March 2017

MKUTANO MKUU MAALUMU CCM MACHI 12

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepanga kufanya Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa, Machi 12, mwaka huu, mjini Dodoma.

Mkutano huo umeitishwa, kufuatia mageuzi makubwa yaliyofanyika ndani ya Chama, yakiwemo marekebisho ya kanuni na Katiba ya CCM.

Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Rodrick Mpogolo, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, mkutano huo utatanguliwa na vikao viwili vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Kwa mujibu wa Mpogolo, kikao cha Kamati Kuu kitafanyika Machi 10, mwaka huu na kufuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Alisema katika mkutano mkuu, pamoja na mambo mengine, wajumbe watapata fursa ya kujadili na kupitisha marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1997 Toleo la 2012, kanuni za Chama na Jumuia zake.

Mpogolo alisema marekebisho hayo yanafanyika, kufuatia maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM, katika kikao chake kilichofanyika Desemba, mwaka jana, Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu alizitaja kazi zingine zitakazofanywa na wajumbe wa mkutano huo kuwa ni kupokea taarifa ya ratiba ya uchaguzi mkuu wa CCM na Jumuia zake, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu kote nchini.
  
“Vikao vyote hivyo vitafanyika mjini Dodoma, ambako ni makao makuu ya Chama kama ilivyo kawaida yetu,"alisema.

Hata hivyo, Mpogolo hakutaja idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu kwa maelezo kuwa, bado wananendelea kufanya uhakiki wa wajumbe ili kupata idadi kamili.

Alisema Chama kimewaagiza viongozi wa wilaya na mikoa, kuwapatia taarifa za idadi ya wajumbe walioko katika maeneo yao ili waweze kujua idadi kamili ya wajumbe watakaohudhuria mkutano mkuu maalumu.
 Mkutano huo utafanyika siku chache baada ya CCM, kufanya maadhimisho ya kutimiza miaka 50, tangu kilipozaliwa, Februari 5, 1977. Maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa mkoani Dodoma.

No comments:

Post a Comment