Tuesday 7 March 2017

WANAFUNZI WAANDAMANA, MABOMU YARINDIMA SIMIYU



ZAIDI ya wanafunzi 600 wa Shule ya Sekondari Bariadi, iliyoko katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, wameandamana na kufunga barabara kuu ya Bariadi –Lamadi, wakipinga kuhamishwa kwa Mkuu wa shule hiyo, Deus Toga.

Mwalimu huyo alikuwa amepata uhamisho kwenda katika shule ya sekondari ya Giriku, iliyoko katika halmashauri hiyo. Uhamisho huo umefanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri, Merkzedek Humbe.

Tukio hilo lilitokea jana, saa tano asubuhi, katika barabara hiyo na kusababisha kusimama kwa shughuli za mji wa Bariadi, kwa muda wa saa mbili.

Wanafunzi hao walianza kuandamana kwenda katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri, lakini hawakufika kutokana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kuzuia maandamano hayo.

Hata hivyo, wanafunzi hao wakiwa katikati ya barabara hiyo, waliamua kuandamana tena kwenda ofisi ya mkuu wa mkoa, jambo lililoshindikana pia baada ya askari hao kuwazuia tena eneo la Hospitali teule ya mkoa ya Somanda.

Baada ya jihudi zao kukwama, wanafunzi hao, ambao ni wa kidato cha kwanza hadi cha sita, waliamua kukaa katikati ya barabara huku wakiimba nyimbo za kushinikiza  kuwa, hawamtaki mwalimu Paul Lutema, ambaye amepelekwa kuwa mkuu wa shule hiyo.

“Hatumtaki Mwalimu Lutema, tunamtaka mwalimu wetu Toga, hatumtaki Lutema,tunamtaka mwalimu Toga,” waliimba wanafunzi hao.

Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kumkataa mwalimu Lutema na kumtaka mwalimu Toga, wanafunzi hao walianza kuwarushia mawe askari hao wakitaka wasiwazuie kwenda ofisi ya mkuu wa mkoa.

Hali hiyo ilisababisha jeshi la polisi kuanza kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi hao, huku wakiwafukuza kurejea katika eneo la shule, ambapo baadhi yao walikamatwa na kupigwa virungu na kuwekwa ndani ya magari ya polisi na kupelekwa kituo cha polisi Bariadi.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wanafunzi hao walisema waliingiwa na mshituko asubuhi ya jana, baada ya kutangaziwa kuwa Mwalimu Toga
amehamishwa.

Walisema baada ya kutangaziwa, waligoma kuingia madarasani na kuamua kuandamana kwenda ofisi ya mkurugenzi na mkuu wa mkoa, wakitaka mwalimu mkuu huyo asihamishwe  kutokana na uchapakazi wake kuwa mzuri tangu amefika katika shule hiyo.

“Toka mwalimu huyu kafika shuleni hapa, ufaulu umeongezeka na migogoro ya shule iliyokuwepo, haipo tena na duka la shule lilikuwa limefungwa kutokana na migogoro ya walimu, lakini tangu amekuja hiyo migogoro imekwisha na duka linafanya kazi,’’ alisema Justine Mshana.

Baadhi ya walimu wa shule hiyo, ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema kuwa wanafunzi hao wasikilizwe kwani madai yao ni ya msingi.

Kutokana na hali hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga na Ofisa Elimu wa Mkoa, Julius Nestory, walifika shuleni hapo kuwatuliza wanafunzi hao.

Kiswaga aliwataka wanafunzi warejee madarasani wakaendele na masomo kwani madai yao yamekubaliwa na kwamba, mwalimu huyo hatahamishwa, badala yake atabaki katika shule hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu, Nestory alisema ofisi ya mkurugenzi ilifanya maamuzi yasiyo sahihi bila kuzingatia sheria na taratibu za uhamisho kwa sababu mwenye mamlaka ya kuwahamisha wakuu wa shule ni katibu tawala wa mkoa.

Alipotafutwa kuzumgumzia hali hiyo, Mwalimu Deus Toga, alikataa kuzungumzia suala hiyo kwa maelezo kuwa yeye hahusiki.

No comments:

Post a Comment