Thursday 9 March 2017

MFANYABIASHARA MAARUFU AJIPIGA RISASI DODOMA


MFANYABIASHARA maarufu wa vinywaji baridi na pombe kali za jumla na rejareja, Festo Mselia, amejiua kwa kujipiga risasi kichwani katika tukio linalohusishwa na ukaguzi uliofanywa kuhusiana na viroba.

Msako huo ulifanywa kufuatia vinywaji hivyo kupigwa marufuku na serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Tukio hilo ambalo linaonekana kuwa na utata, limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mjini hapa, katika eneo la Area D nyumbani kwa marehemu, ambako ndipo msiba upo, muuzaji mkuu wa duka la Mselia, Leslier Msigwa, alisema tukio hilo linahusishwa na shehena ya viroba vilivyokuwa katika duka la marehemu.

Alisema marehemu alijipiga risasi katika shamba lake lililoko eneo la Msalato, nje kidogo ya Mji wa Dodoma, ambako ni zaidi ya kilomita 25, kutoka katikati ya mji.

Msigwa alisema taarifa hizo alizipokea baada ya mdogo wake wa marehemu aitwae David Mselia, kumpigiwa simu kutoka Arusha na askari, ambaye alidai kaka yake amejipiga risasi.

Msigwa alisema, Ijumaa iliyopita, marehemu alikamatwa na askari kwa madai ya kuuza viroba katika duka lake lililoko barabara ya 11.

Alisema marehemu alipata dhamana, lakini aliambiwa arudi Jumatatu, jambo lililomfanya kubaki kuwa mtu mwenye mawazo baada ya kukamatwa na polisi.

"Alikuwa akiniuliza kila mara kuhusiana na suala la viroba linaendeleaje na kuna siku tulikuwa tunaangalia taarifa ya habari, tukaona habari ya kukamatwa kwa viroba katika eneo la Tegeta, akanambia unaona wale wamekamtwa wenye tani nyingi, sisi tuna hivi vidogo tu hatuwezi kukamatwa,’’ alisema.

Msigwa alisema Ijumaa. walifika dukani saa tatu asubuhi na kuendelea na biashara kama kawaida na ilipofika saa sita, mke wa Mselia afika dukani hapo.

“Alipofika majira ya mchana, nilimwambia mama tunatakiwa kwenda benki, ambao ni utaratibu wetu wa kila siku kupeleka fedha, mama akasema baba yako umempigia? Nikamwambia sijampigia, yeye akampigia, baba alimjibu subiri mpaka nije, lakini hakufika mpaka muda wa benki ukaisha na hatukupeleka fedha kwa siku hiyo,”alisema.

Aliongeza kuwa kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine, aliondoka mapema siku hiyo na kuendelea na ratiba iliyokuwa mbele yake.

Msigwa alisema mpaka kufika saa moja usiku, akiwa amekaa kwenye baa ya Green Land, iliyoko jirani na nyumbani kwake, ambayo marehemu alikuwa anaimiliki na walikuwa na utaratibu wa kupita hapo kabla ya kufika nyumbani, hakumuona marehemu na kuamua kumpigia simu ili ajue alipo.

Muuzaji huyo alisema simu yake iliita bila majibu, ambapo alihisi marehemu huenda alikuwa nyumbani anakoga kwa muda huo, jambo ambalo halikuwa sawa.

Alisema ilipofika saa mbili usiku, alipokea simu kutoka kwa mdogo wake marehemu aliyeko  Arusha, ambaye alimwambia mbona anampigia simu Chola, lakini hapokei.

“Nilichukua uamuzi wa kumpigia simu, nikimfahamisha kuwa anatafutwa na kwamba hapokee simu yake, ambapo alinijibu kuwa alikuwa anapiga simu nyingine, ambayo nilikuwa nayo mbali, lakini akanimbia kuna taarifa kwamba kuna mfanyabiashara maarufu Dodoma amejipiga risasi,”alisema.

SHAMBANI KWA MAREHEMU.

Uhuru ilifanya jitihada za kufika shambani kwa marehemu, ambapo ndipo inaposemekana alijipigia risasi na kuzungumza na mtunza shamba aliyejitambulisha kwa jina la Baraka John.

John, ambaye ndiye mtu wa kwanza kufika katika eneo la tukio na kushuhudia mwili wa bosi wake ukiwa na majeraha, alisema wakati tukio linatokea, alikuwa anatokea porini kuchunga mifugo.

Alisema baada ya kufika nyumbani anakoishi, alimkuta mzee mmoja wa makamo, ambaye aliongozana na marehemu.

John alisema mzee huyo alimwagiza achukue baiskeli amfuate marehemu shambani kwani alimwambia amsubiri na amemsubiri kwa muda mrefu, hajarudi.

“Nilichukua baiskeli na kwenda shambani kwa ajili ya kumwangalia marehemu, nilipofika shambani nilizunguka nikimtafuta bila mafanikio. Nilianza kukata tamaa, lakini nilipoangalia pembeni ya mti mkubwa, nilimwona akiwa amelala chini,’’alisema kijana huyo.

"Alikuwa akihangaika na damu nyingi zikimtoka. Nikapata mshtuko na kugeuza baiskeli yangu na kwenda kumwambia yule mzee na majirani. Yule mzee alipiga simu polisi na wale majirani niliowaambia, walitoa taarifa kwa diwani, mtendaji na mwenyekiti wa kijiji, ambapo baada ya muda walifika na kwenda eneo la tukio,”alisema.

Alisema baada ya muda, yalifika magari mawili ya polisi, ambao walimbemba majeruhi Mselia.

“Walipofika hapa nyumbani ninakoishi, askari waliomba godoro ambapo niliwapa na kumbebea majeruhi huku damu nyingi zikiwa zinamtoka,"alisema.

ALIYEKUWA NAYE DAKIKA ZA MWISHO

Rafiki wa marehemu, Jonas Mazengo, alisema marehemu alifika nyumbani kwake saa 3.00 asubuhi juzi.

“Alinikuta naoga, akakaribishwa, nilipomaliza mke wangu aliniambia kuna mgeni wangu nje ananisubiri,”alisema.

Alisema alimweleza jinsi alivyokamatwa na viroba vya pombe na kwamba anadaiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia.

“Tuliongea mambo mengi, lakini baada ya muda ilipigwa simu na akaipokea na kuongea nayo. Alivyokata akaniambia kuwa amepigiwa na RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) aende kituoni, lakini nimemwambia kuwa nitakwenda saa 9.00 jioni, kwa sababu bado niko shambani. Ama twende saa hizi?” Alisema.   
Alisema alimwambia kuwa wasiende wakati huo kwa sababu alishamwambia kuwa yupo shambani na kwamba angekwenda baadaye.

“Alinikubalia, tukasubiri chakula na tukala kisha tukaenda polisi. Tulipofika tukamkuta RCO anakagua gari moja lililokuwa na wahamiaji haramu na kisha akatuambia kuwa tumsubiri RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma),”alisema.

Alisema baadaye RPC alifika na wakaenda katika stoo kulikohifadhiwa viroba na kisha walimruhusu aondoke na kwamba, wakimhitaji watamwambia.

“Tuliondoka pale na kwenda shambani kwake Msalato, tukiwa ndani ya Prado, ambayo aliniambia niendeshe mimi,”alisema.

Alisema walipofika katika shamba, ambalo hutumia kufuga mifugo yake alimwacha na kwenda kumtafuta kijana anayewatunza.

Hata hivyo,  alisema hadi ilipofika saa 12.00 jioni, alikuwa hajafika ingawa kijana anayechunga alikuwa amefika.

“Nilimwambia aende akamfuatilie mzee, lakini baada ya muda mfupi alirudi na kuniambia amemkuta anagaragara huku damu zinatoka na bastola ipo pembeni,”alisema Mazengo.

Alisema walikwenda na kukuta akiwa anatapatapa, simu na gari viko pembeni.


KAULI YA KAMANDA

Akizungumza kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Mambosasa alisema walimkamata marehemu Machi 3, mwaka huu, kutokana na kufanya biashara ya viroba.

“Hayo wanayosema ya kujiua kutokana na viroba mimi sijui ila ninachokijua ni hicho nilichokueleza,” alisema Mambosasa

Alisema walipofika dukani kwake  walikuta kuna shehena ya katoni 1,269 za viroba.

No comments:

Post a Comment