Thursday 9 March 2017

MAKONDA AWA GUMZO DAR, ATOA SALAMU NZITO KUHUSU DAWA ZA KULEVYA


KITENDO cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kushindwa kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, jana, ambapo ilipangwa awe mgeni rasmi, kimezua gumzo zito miongoni mwa wananchi.

Makonda alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, ambayo kimkoa yalifanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke.

Umati mkubwa wa wanawake ulifurika katika viwanja hivyo huku wananchi wakiwemo wapita njia, wakionekana kuhudhuria baada ya kupata taarifa kwamba mgeni rasmi  angekuwa mkuu huyo wa mkoa.

Asilimia kubwa ya wananchi walikuwa na shauku ya kumuona na kumsikiliza mkuu huyo wa mkoa, ambaye amekuwa gumzo kubwa hapa nchini kutokana na umachachari wake katika utendaji, mikasa inayomzunguka na mijadala katika mitandao ya kijamii.

Pia, kumekuwa na mashambulizi dhidi yake yanayoendelea kutolewa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambayo yamewafanya wananchi wengi kuwa na shauku kubwa ya kumuona na kumsikia.

Sababu nyingine inayofanya wananchi kuwa na kiu ya kumuona na kumsikiliza ni vita aliyotangaza dhidi ya dawa za kulevya, ambayo aliapa kuendelea nayo hadi mambo yakae sawa.

Mbali ya hayo, mitandao ya kijamiii imekuwa ikieleza na kumuonyesha Makonda kuwa amekwenda Afrika Kusini.

Licha ya mvua iliyokuwa ikinyesha jana, wanawake na wananchi wengi waliendelea kubaki uwanjani hapo, wakiwa na shauku ya kumuona Makonda.

Hata hivyo, upepo ulibadilika ghafla baada ya mshereheshaji wa maadhimisho hayo kutangaza kuwa, mgeni rasmi alikuwa anaingia uwanjani hapo.

Macho ya wengi yalielekezwa eneo, ambalo mgeni rasmi alikuwa akiingilia, ambapo baada ya kushuka, ilibainika alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva.

Hali hiyo ilizua gumzo kubwa huku watu wakibishana na kuhoji alipo Makonda, ambaye katika kipindi kifupi cha uongozi wake mkoani Dar es Salaam, amefanikiwa kuibua mambo tofauti, ikiwemo kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Mjadala wa Makonda kutoonekana uliendelea hata kwa waandishi wa habari,  ambao wengi walikuwa katika hali ya sitofahamu huku wakionekana kufika hapo kwa ajili ya kuthibitisha tu kama angehudhuria au la.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Theresia Mbando, aliwaeleza wananchi kuwa, Makonda alikuwa na dharura, hivyo alimtuma Lyaniva ili amwakilishe.

“Ilitakiwa mkuu wetu wa mkoa ndiye awe mgeni rasmi hapa, lakini ana dharura, hivyo anawakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Lyaniva,” alisema Theresia.

Naye Lyaniva aliwaambia wananchi kwamba, alimwakilisha mkuu huyo wa mkoa kutokana na dharura.

“Yuko katika majukumu mengine, hivyo amenipa hotuba yake niisome na nitaisoma kama ilivyo.

"Lakini alisema kabla sijasoma hotuba hii, niwaambie mambo mawili. Mkuu wa Mkoa amenituma niwaambie anawapenda sana. Jambo la pili amesema kwa watoto, ambao bado hawajazaliwa, hakuna atakayekufa au kuathirika na dawa za kulevya,”alisema Lyaniva.

No comments:

Post a Comment