Thursday, 9 March 2017

VIGOGO WATATU WALIOTIMULIWA CCM WAREJESHWA


VIGOGO watatu wa CCM waliofukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kukisaliti Chama kwenye uchaguzi mkuu, wamerejeshewa uanachama wao mpaka hapo Kamati Kuu ya CCM itakapoamua vinginevyo.

Vigogo hao ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Wilfred Soilei, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Wilaya ya Arumeru, Mathias Manga na Mjumbe wa NEC kutoka Wilaya ya Meru, Julius Mungure.

Akithibitisha kurejeshewa uanachama wao, Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa wa Arusha,  Omary Bilali, alisema ni kweli amepata barua kutoka Makao Makuu ya CCM ya kuitaka CCM Mkoa wa Arusha kuwarejeshea wanachama hao uanachama wao.

Bilali alisema wajumbe hao watatu mamlaka ya mwisho ya kuwafukuza uanachama ni Kamati Kuu ya CCM kutokana na nyadhifa zao.

"Baada ya kupata maelekezo kutoka makao makuu, ofisi yangu imewaandikia barua wanachama hao ya kubatilisha barua zao za awali za kuwafukuza uanachama wa CCM," alisema Bilali.

Akizungumza na Uhuru, akiwa njiani kwenda Dodoma, Mungure alikiri kupokea barua ya kufukuzwa uanachama wa CCM, lakini hakuridhika na maamuzi hayo hivyo aliamua kukata rufani.

"Juzi nilipigiwa simu na Katibu Bilali kunijulisha kuwa nahitajika Dodoma, sijui ninaitiwa kitu gani. Lakini ni sehemu ya maelekezo ya Chama changu kwamba, nikifika huko nitajua ninachoitiwa,"alisema Mungure

Kwa upande wake, Manga alisema yupo msibani Kibosho na kwamba, hawezi kuzungumzia suala hilo na kuahidi kumtafuta mwandishi wa habari hizi baada ya kumaliza shughuli za mazishi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Soilei alikiri kupokea barua ya kufukuzwa uanachama na kwamba, jana alipata barua kutoka ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha ya kubatilisha barua yake ya kufukuzwa uanachama.

Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa iliyofanya kikao chake Februari 11, mwaka huu, iliwafukuza wanachama 1,520, waliokisaliti Chama katika uchaguzi mkuu wa 2015.

No comments:

Post a Comment