Thursday, 9 March 2017

UMOJA WA MATAIFA WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI



KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, amesema ana matumaini makubwa ya maridhiano nchini Burundi kupitia Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Dk. John Magufuli.

Pia, ameisifu Tanzania kwa uwezo wake mkubwa wa kutekeleza na kusimamia kanuni za utawala bora, kama vile kudumisha amani na kujenga mazingira ya amani katika EAC na Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Guterres alisema hayo wakati alipowasili nchini, akitokea Somalia na Kenya, kwa ziara ya kikazi na kukutana na mwakilishi wa Rais Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga.

Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, ilitoa wito kwa Katibu Mkuu huyo kuendelea kutoa msaada kwa lengo la kuleta utulivu wa kisiasa nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Ujumbe huo ulieleza kuwa, kukosekana kwa hali ya utulivu hivi karibuni katika nchi hizo mbili, kumesababisha kutokea kwa kasi ya kufurika kwa wakimbizi Tanzania na nchi za jirani, hivyo ni jukumu la UN kuhakikisha hali ya utulivu inarejea.

Akitoa ujumbe wa Dk.Magufuli, Waziri Mahiga alisema Tanzania ina matumaini makubwa ya kupatikana kwa maridhiano katika mgogoro huo.

“Maridhiano haya yanaongozwa chini ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda na kuwezeshwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na kwamba, mkutano ujao wa jumuia hiyo ya EAC unatarajiwa kupokea ripoti za maendeleo kuhusu mchakato huo,”alisema.

Balozi Mahiga alisema Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ipo pia kwenye SADC, ambapo madhumuni yake makubwa ni mabadiliko ya kisiasa nchini humo.

Alisema wanachama wa jumuia hiyo ya SADC wanatarajia kufanya maamuzi mazuri  kuhusu hatma ya nchi ya Congo na kwamba, Tanzania ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC, ambapo ndani yake kuna chombo cha kisiasa, ulinzi na usalama.

“Hivyo kama nchi yetu ni mwenyekiti wa sasa, ni dhahiri kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa msaada wa mafanikio katika maridhiano hayo, kudumisha hali ya amani na usalama kama sehemu ya kuheshimu utawala wa sheria katika kanda hiyo ya SADC,” alisema.

Guterres alipongeza juhudi za Rais Magufuli katika kutafuta hali amani na kwamba, anaonyesha utayari wake kwa kukaribisha idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Burundi.

"Umoja wa Mataifa unashukuru kazi iliyofanywa na Rais mstaafu Mkapa katika usuluhishi nchini Burundi chini ya jumuia ya EAC na uongozi wake na kwamba nina uhakika watafanikiwa kupata ufumbuzi wa kudumu,"alisema.

Waziri Mahiga aliwaambia waandishi wa habari kwamba, Rais Magufuli alikutana na Guterres wakati wa Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu, ambapo viongozi hao walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu jumuia za kikanda.

"Rais Magufuli aliniagiza kufikisha ujumbe wake kwa Katibu Mkuu Guterres, na pia kumualika wakati muafaka akiwasili kwenye ziara ya kikazi nchini," alisema.

Guterres alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mahiga, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JIA), jana usiku, akitokea nchini Somalia na Kenya kwa ziara ya kikazi.

Pia, alipokelewa na Mratibu Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez na Mkurugenzi wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Balozi, Celestine Mushy.

No comments:

Post a Comment