Thursday, 9 March 2017

TANESCO YACHACHAMAA, YATOA SIKU 14 KWA WADAIWA SUGU KULIPA MADENI

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limetoa siku 14 kwa wadaiwa sugu kuhakikisha wamelipa madeni yao, vinginevyo watasitishiwa huduma hiyo.

Aidha, TANESCO imesema inawadai wateja wake sh. bilioni 275.381, hadi kufikia Januari, mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Tito Mwinuka, alisema jana, Dar es Salaam kuwa, wanatoa siku 14, baada ya hapo TANESCO watasitisha huduma kwa wateja wanaoshindwa kulipa madeni yao na hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa.

"TANESCO inautaarifa umma na wateja wake wote kwa ujumla kuwa, inakusudia kuendesha zoezi kabambe la ukusanyaji wa madeni ya bili za umeme zilizolimbikizwa na wateja mbalimbali. Madeni hayo yanajumuisha wateja wadogo, wizara, taasisi za serikali na kampuni binafsi," alisema.

Aliyataja madeni yanayodaiwa kwa wizara na taasisi za serikali kuwa ni sh. bilioni 52.534, kampuni binafsi na wateja wadogo sh. bilioni 94.973, wakati Shirika la Umeme la Zanzibar (ZESCO) sh. bilioni 127.873.

Mwinuka alisema malimbikizo ya madeni yamekuwa yakikwamisha jitihada za utekelezaji wa majukumu ya msingi ndani ya shirika kwa wakati.

Kutokana na madeni hayo kushindwa kulipwa, alisema shirika linashindwa kufanya majukumu yake kama shughuli za uendeshaji wa shirika, matengenezo ya miundombinu na utekelezaji wa miradi.

"Ni matarajio yangu kuwa, kulipwa kwa malimbikizo haya ya madeni, kutasaidia TANESCO kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi mkubwa zaidi na hivyo kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta zinazotegemea nishati ya umeme hapa nchini," alisema.

Wiki iliyopita, Rais, Dk. John Magufuli, aliiagiza TANESCO kuwakatia umeme wateja wote wenye madeni makubwa, ikiwemo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Rais Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha TANESCO, mkoani Mtwara, ambapo alisema taasisi zote za umma zinapaswa kulipa madeni la sivyo zitakatiwa umeme.

Alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kutoogopa kwa sababu umeme unapaswa kukatwa hata Ikulu kama utakuwa haujalipiwa.

No comments:

Post a Comment