Thursday, 4 August 2016

MWAMBALASWA, LUGOLA, MURAD WAACHIWA HURU




WABUNGE watatu waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za kuomba rushwa, wameachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuwasilisha hati ya kuwaondolea mashitaka.
Wabunge hao, Kangi Lugola (Mwibara – CCM), Victor Mwambalaswa (Lupa – CCM) na  Suleiman Sadiq Murad (Mvomero –CCM), waliachiwa huru jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage.
Wabunge hao wakiwa na nyuso za furaha baada ya kuachiwa huru, walisema Mwenyezi Mungu ametoa majibu kwa wao kuachiwa huru kwa kuwa walijua tangu mwanzo kesi hiyo ilikuwa ya kutunga na kutengeneza kwa sababu za kisiasa.
Awali, wabunge hao ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 31, mwaka huu, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mwijage, wakati shauri hilo lilipokwenda kwa usikilizwaji wa awali.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kwa kushirikiana na Wakili wa TAKUKURU, Emmanuel Jacob, alidai shauri lilikwenda kwa usikilizwaji wa awali.
Alidai, hata hivyo DPP hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya washitakiwa chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Baada ya kuwasilisha hayo, Wakili wa utetezi, Mpare Mpoki, aliomba kupatiwa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo na baada ya upande wa jamhuri kuomba kuondoa mashitaka.
Hakimu Mwijage alisema shauri linaondolewa mahakamani kama ilivyoombwa na upande wa jamhuri na washitakiwa wanaachiwa huru.
Kuhusu ombi la wakili wa utetezi, Hakimu Mwijage alisema wakili huyo afanye juhudi kufuatilia upande wa jamhuri maelezo hayo kwani kwa mujibu wa sheria, mahakama haiwezi kuamuru upande huo umpatie kwa hatua ya kesi ilipofikia.
TAKUKURU IMETUDHALILISHA
Akizungumza kwa niaba ya wenzake baada ya kuachiwa huru, Lugola alisema kimsingi tangu walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, moyoni mwao walianza na Mwenyezi Mungu na kuahidi kumaliza naye.
“Leo (jana) Mwenyezi Mungu ametoa majibu kwamba tumekuwa huru. Tunawaambia Watanzania, kesi hii tulijua tangu mwanzo ya kutunga na kutengenezWa kwa sababu za kisiasa,” alisema Lugola.
Alisema serikali kupitia TAKUKURU, hawakuwa na ushahidi, ndiyo maana wanakuwa vinyonga na vigeugeu kwa kuwa walisema upelelezi tayari, mara wanaifuta.
Hata hivyo, wabunge hao walisema sasa ni muda wao wa kuwatumikia wananchi majimboni kwao na watakaa na mwanasheria wao kutafakari la kufanya kutokana na udhalilishaji waliofanyiwa na TAKUKURU.
“Baada ya kushauriana na wanasheria tutajua nini cha kufanya, lakini tumesikitishwa na udhalilishaji tuliofanyiwa na TAKUKURU,” alisema mbunge huyo.
Wabunge hao  Murad (53), Lugola (54) na  Mwambalaswa (63), walikuwa nje kwa dhamana tangu walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, kujibu tuhuma za  kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Hati ya mashitaka ilionyesha kuwa, wabunge hao walikuwa wakidaiwa kutenda kosa hilo Machi 15, mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne usiku, katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyoko Masaki, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Ilidaiwa wabunge hao wakiwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), walishawishi au kuomba rushwa ya sh. milioni 30, kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Mbwana Magotta.

Walidaiwa kwamba waliomba rushwa hiyo kama kushawishi cha kutoa mapendekezo mazuri ya hesabu za fedha za halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/16.

No comments:

Post a Comment