Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MKE wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma
Kikwete, amewataka wapigakura wa Jimbo la Chalinze, wasidanganyike na kutofanya
makosa ya kuwachagua wapinzani, badala yake wawachague wagombea wa CCM.
Mama Salma, ambaye pia ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, amewaomba wananchi hao kumchagua Dk. John
Magufuli kuwa rais, Ridhiwani Kikwete kuwa mbunge na madiwani wote kutoka CCM.
Amesema maendeleo ya kweli na ya
haraka huletwa na viongozi kutoka ndani ya CCM na kwamba, ndio wenye uwezo na
sifa za uwajibikaji.
Aliyasema hayo juzi jioni, wakati
akizungumza kwenye mkutano wa kampeni za Ridhiwani, katika Kijiji cha Pera,
Jimbo la Chalinze, ambapo alisema wana-Chalinze hawapaswi kuharibu kura kwa
kuwapa wapinzani.
“Uongozi si lelemama ndugu zangu, hawa
wenzetu wa upinzani bado hawajui lolote ni wababaishaji. Tumchague Dk. Magufuli
na Ridhiwani kuwa mbunge wetu kwa sababu ndio wenye sifa za uongozi.
“Huyu Ridhiwani ni mtoto wenu na
hajaanza kuisaidia Chalinze leo hivyo, tuendelee kumuunga mkono ili atusaidie
zaidi kuinua maendeleo yetu,” alisema.
Naye Subira Mgalu, ambaye ni mbunge mteule
wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, alisema Ridhiwani anatosha kuendelea kuongoza
jimbo hilo kutokana na kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2010 kwa mafanikio
makubwa.
Alitumia fursa hiyo kuwataka vijana, wanawake
na wazee kujitokeza kwa wingi wakati wa kupigakura na kumchagua Dk. Magufuli
kuwa rais na Ridhiwani kuwa mbunge ili washirikiane kuleta maendeleo.
No comments:
Post a Comment