NA
THEODOS MGOMBA, CHILONWA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma, kimesema hakuna mtu mwenye uwezo wa kusimama na kujigamba kuwa amemsaidia mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli.
Amesema
kama kuna mtu wa aina hiyo ni mzushi na atakuwa anajipendekeza na anastahili
kupuuzwa hadharani kwa kuwa, Dk. Magufuli ameteuliwa kutokana na sifa zake
kiutendaji na uadilifu wakati wote akiwa ndani ya serikali.
Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, wakati akizindua kampeni za Chama katika Jimbo la
Chilonwa.
Katika mkutano huo, Kimbisa alisema moja ya sifa za Dk.
Magufuli ni mtu ambaye hana makundi wala makandokando katika utumishi
wake.
“Siwezi kumnadi mtu ambaye simjui, lakini Dk. Magufuli namfahamu utendaji wake, ni mtu ambaye hana makundi, muadilifu na aliingia katika kusaka nafasi ya uteuzi akiwa yeye na Mungu wake kutokana na uadilifu wake,’’ alisema Kimbisa.
Alisema kuna kila umuhimu wa kumpigia kura mgombea huyo
wa urais kupitia CCM kwani uwezo wake kiutendaji unastahili sifa na ataweza
kulipeleka taifa mbele kutoka hapa lilipo.
“Hakuna mtu mbaye atatoka kifua mbele kuwa eti alimsaidia ili ateuliwe, hakuna bali ni sifa alizonazo na umahiri wake katika kazi, hivyo tumpigie kura nyingi,’’ alisisitiza.
Alisema kutokana na
utendaji wake, mgombea huyo ana deni na wananchi na kwamba ni mpambanaji
na muadilifu.
Kimbisa alisema wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, ameweza kufanya kazi nzuri katika ujenzi wa barabara nchi nzima na kwa sasa zinapitika kwa kiwango cha lami.
“Sasa kama alipokuwa waziri aliweza kufanya hayo yote, tukimpa urais si ndiyo mambo yatanyooka zaidi kuliko ilivyo sasa,’’ alisema Kimbisa.
Akimnadi mgombea wa Jimbo la Chilonwa, Joel Mwakanyaga kupitia CCM, Kimbisa alisema mgombea huyo ana sifa ya uvumilivu kwani katika miaka mingi aliyogombea jimbo hilo na kukosa, hakuwahi kukihama chama.
Alisema ni haki yake sasa kupewa nafasi hiyo kwani katika kipindi chote aliendelea kuwa pamoja na Chama kama vile hakuna jambo lililotokea.
Naye mgombea huyo akiomba kura kwa wananchi wa jimbo
hilo, alisema hatafanya jambo lolote nje ya utekelezaji wa Ilani ya Chama.
Aliahidi kuwa karibu na wananchi katika kutatua changamoto zao na kulililetea jimbo hilo maendeleo.
No comments:
Post a Comment