Sunday, 20 September 2015

CCM YAMUONYA MAALIM SEIF




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemuonya mgombea urais wa chama cha CUF, Maalim Seif Sharifu Hamad, kuacha ‘chokochoko’ na badala yake afanye kampeni za kistarabu bila ya kuwagawa wananchi.

Aidha, kimesema viongozi wa chama hicho wameanza kugombana baada ya kuona mikutano ya mgombea urais wa Chama, Dk. Ali Mohammed Shein, imefanikiwa vilivyo kisiwani Pemba.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema hayo jana, katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Shein, uliofanyika wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema Maalim Seif ameanza ‘chokochoko’ kutokana na wafuasi wake kuwashambulia wana-CCM na kuharibu magari yanayokwenda kwenye mikutano ya Chama.

Vuai alisema pamoja na kutia saini makubaliano maalumu ya uchaguzi ambayo ni pamoja na kufanya kampeni kwa ustaarabu, wafuasi wa CUF, wameanza vurugu kwa kuwashambulia wana-CCM na kuchana picha za wagombea wa CCM.

Alisema hila hizo zinafanywa na Maalim Seif ambaye ameshindwa kuwadhibiti wafuasi wake na kwamba Chama kinamtaka afanye kampeni za kistaarabu.

Kwa mujibu wa Vuai, viongozi wa CUF, wameanza kulumbana baada ya kuona mikutano ya Dk. Shein, inafanikiwa vilivyo kisiwani Pemba.

Alisema Dk. Shein amefanya mikutano mitatu ya kampeni kisiwani humo ambayo maelfu ya wananchi na wana-CCM walijitokeza kumsikiliza.

Vuai alisema viongozi hao wa CUF juzi, walikuwa na kikao cha dharura kujadili namna wanavyoweza kuwazuia watu kwenye mikutano ya CCM.

“Hivi sasa CUF wameanza kulumbana baada ya kuona mikutano yote ya mgombea wetu (Dk. Shein), wananchi wanajitokeza kwa wingi. Waliweka kikao na kuulizana kuwa pamoja na kugawa vespa kila jimbo, lakini hazijasaidia kuwazuia watu wasihudhurie mikutano ya CCM,” alisema.

Alisema mwaka huu, CUF imeshikwa pabaya baada ya kuwadanganya watu kwa miaka mingi na kwamba CCM itapata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Ramadhani Abdallah Shaabani, alisema mwaka huu, Dk. Shein ana kila sababu ya kushinda kutokana na mambo mengi ya maendeleo aliyofanya.

Akizungumzia suala la mafuta na gesi, alisema anawashanga CUF, kuidandia hoja ambayo hawaifahamu na kwamba suala hilo limeshapatiwa ufumbuzi.

Shaabani alisema suala hilo limo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na tayari linafanyiwa kazi kwa nguvu zote ikiwa ni pamoja na kuingia makubaliano ya awali.

Aliwataka CUF kuacha kudandia mambo ambayo hawayafahamu na kwamba sheria ya mafuta na gesi imeshaanzishwa, ambapo katika baraza la wawakilishi lijalo, muswaada huo utawasilishwa ili uweze kupitishwa na kuwa sheria.

Shaabani alisema Zanzibar itakuwa na mamlaka kamili ya kuchimba na kutafuta nishati hiyo na mapato yatakayopatikana yatawanufaisha wananchi na serikali kwa ujumla.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, alisema mwaka huu, lazima CCM ipate majimbo kisiwani Pemba.

Alisema wananchi wa kisiwa hicho wana kila sababu ya kuwachagua wagombea wa Chama kutokana na mambo mengi yaliyofanyika katika utawala wa Dk. Shein.

0000

No comments:

Post a Comment