HABARI ZOTE NA MOHAMMED ISSA,
MICHEWENI
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema iwapo atapewa ridhaa ya
kuiongoza tena Zanzibar, atahakikisha visiwa hivyo vinakuwa eneo huru la
uwekezaji na viwanda.
Amesema serikali yake imetenga
maeneo huru kwa ajili ya uwekezaji Unguja na Pemba kwa lengo la kuvibadili
visiwa hivyo na kukuza uchumi wa wananchi na taifa.
Mgombea huyo alisema hivi sasa kuna
mwekezaji ameonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda cha sukari katika wilaya ya
Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.
Aidha, alisema katika awamu ya pili
ya utawala wake, ataboresha sekta ya uvuvi na kuwa ya kisasa ili iweze
kuwanufaisha wananchi na kukuza pato la taifa.
Dk. Shein alisema alisema hayo jana,
katika mkutano wake wa tatu wa kampeni kisiwani Pemba, uliofanyika wilaya ya
Micheweni na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi na wana-CCM.
Dk. Shein tayari amefanya mikutano
ya kampeni katika wilaya ya Chake Chake mkoa wa Kusini, Konde na Micheweni mkoa
wa Kaskazini, Pemba.
Alisema atahakikisha Zanzibar
inakuwa eneo huru la uwekezaji na viwanda na kwamba tayari maeneo ya uwekezaji
yametengwa na wakati wowote yataendelezwa.
Dk. Shein alisema kwa Unguja,
wametenga eneo la Fumba na Pemba wilaya ya Micheweni, ambapo maeneo hayo
yatakuwa mahususi kwa uwekezaji ili kuboresha maisha ya wananchi na serikali
kupata mapato.
Mgombea huyo alisema mpango huo
utaanza wakati wowote na tayari wilaya ya Micheweni kuna mwekezaji ameonyesha
nia ya kutaka kujenga kiwanda cha sukari na kitakapokamilika kitatoa ajira kwa
vijana.
Alisema eneo la Fumba, tayari
mfanyabiashara Said Salumu Bakharesa ameonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda
cha maziwa ambacho kitakuwa kikubwa katika nchi za Afrika Mashariki.
Dk. Shein alisema katika awamu ya
kwanza ya utawala wake, alianzisha wizara maalumu ya mifugo na uvuvi kwa ajili
ya kuiboresha sekta hizo.
Alisema dhamira yake ni kuhakikisha
sekta ya uvuvi inaboreshwa zaidi na kuwa ya kisasa ili kuwanufaisha wananchi na
taifa kwa ujumla.
Alisema tayari watu kadhaa
wameonyesha nia ya kutaka kujenga viwanda vya samaki Unguja na Pemba na kwamba
hilo likifanikiwa, litaifanya sekta hiyo kuimarika na kuwanufaisha wananchi.
Dk. Shein alisema baada ya kuingia
madarakani, sekta ya uvuvi imekuwa na mafanikio makubwa, ambapo katika kipindi
cha miaka minne na nusu, tani 148,535, za samaki zilivuliwa na kuiingizia
serikali sh. bilioni 532.
Aidha, alisema serikali ya Korea
Kusini, ilileta vifaranga vya samaki ambapo walianzisha mabwawa sita ya kufugia
samaki na kuwafundisha wananchi namna ya kufuga samaki.
“Najuwa wananchi wengi wa Micheweni
na maeneo mengine mnategemea uvuvi, hivyo mkinichagua nitaiboresha sekta hiyo
ili kuwa ya kisasa, itakayowanufaisha na kujipatia kipato,” alisema.
Alisema hivi sasa kuna vikundi vidogo
vidogo vya uvuvi 167, vyenye wanachama 36,000.
Dk. Shein alisema dhamira yake ni
kuibadilisha wilaya ya Micheweni ili kuwa tofauti na ilivyo sasa.
Alisema katika wilaya hiyo, huduma
muhimu za jamii zimeboreshwa ikiwa ni pamoja na kujengwa barabara, umeme na
maji.
Kuhusu Hospitali ya Micheweni,
alisema itapandishwa hadhi na kuwa ya wilaya ambapo itawekewa vifaa vya kisasa.
Alisema baada ya kuingia madarakani,
alihakikisha huduma za uzazi zinatolewa bure kwenye hospitali zote za serikali.
Dk. Shein alisema atahakikisha sekta
ya utalii inaboreshwa zaidi ili kukuza pato la taifa na kuwa mbadala wa kilimo.
Aliwaomba wananchi wamchague kuwa
rais pamoja na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John
Magufuli, wabunge, wawakilishi na madiwani.
Mgombea huyo alisema mwaka huu,
Chama kitapata ushindi mkubwa kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
CCM, ulivyofanikiwa visiwani humo.
No comments:
Post a Comment