Sunday, 20 September 2015

MBATIA ANALINDA MASLAHI GANI KWA LOWASSA?




MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha NCCR - Mageuzi, James Mbatia, hatimaye amejipachika rasmi jukumu la kuwa ni ‘msemaji’ wa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.
Tayari hali hiyo pia imemkera Makamu Mwenyekiti wa NCCR - Mageuzi, Leticia Mosore, aliyesema wiki iliyopita kuwa, Mwenyekiti wake huyo amejigeuza kuwa msemaji wa Chadema, na kwamba amekisahau na kukiacha chama chake hicho mwenyewe kikidhoofika.
Kutokana na hali hiyo, Mosore alimtaka bosi wake kuacha kuisemea Chadema (na Lowassa), badala yake afanyekazi za kuijenga NCCR – Mageuzi, ikiwemo ya kuitisha na kuongoza vikao vya chama chake hicho.
Makamu Mwenyekiti huyo alitoa tuhuma hizo jijini Dar es Salaam, mbele ya waandishi wa habari, akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Mosena Nyambabe.
Karibu wiki nne zilizopita, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa genge linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alijitokeza hadharani mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kumtetea Lowassa kutokana na tuhuma za ufisadi dhidi yake.
Katika kufanya hivyo, mwanasiasa huyo anayegombea ubunge wa jimbo la Vunjo, Moshi mkoani Kilimanjaro, alikwenda mbali zaidi kwa kutaka iundwe Tume ya Maridhiano na Mafisadi ili wasifungwe jela!
Hatua yake hiyo ilikuja siku mbili tu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, kuanika hadharani ufisadi wa Lowassa kuhusu sakata la kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond Development LLC.
Siku kadhaa zilizopita, Mbatia yuleyule na kwa kutumia mtindo uleule wa vyombo vya habari, safari hii kwa kuongea 'live' na wananchi kupitia vituo kadhaa vya televisheni nchini, alimtetea Lowassa kwa ujinga aliofanya akiwa Tabora, wakati wa kampeni zake za urais.
Akiwa kwenye ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mjini humo, Lowassa aliwaomba waumini wa dhehebu hilo nchini kote, wamchague kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa vile wote waliotangulia hakuna hata mmoja kati yao ambaye ni Mlutheri!
"Naomba mniombee, mniombee kwelikweli. Nyie Walutheri mna sababu ya kuomba zaidi kwa sababu tangu nchi hii iumbwe haijapata Rais Mlutheri. (Hayati) Mwalimu (Julius Kambarage) Nyerere alikuwa Mkatoliki, (halafu) Rais (Benjamin) Mkapa (naye) alikuwa Mkatoliki", alisema kwa kinywa chake mwenyewe na kuongeza:
"Sasa nadhani Mungu atatuongoza ili nasi (Walutheri) tuweze kuipata nafasi hiyo. Kwa hivyo naomba mniombee sana," (mwisho wa kunukuu).
Hivyo ndivyo Lowassa alivyosema alipopewa fursa hiyo muhimu ya kusalimia kanisani, nafasi aliyoipata kwa vile alikuwa akisali kwa mara yake ya kwanza kanisani hapo.
Alipewa kwa vile ni utaratibu maalumu wa kanisa hilo kuwatambulisha, wakati wa matangazo waumini wote wageni wanaokuwa na vyeti vya utambulisho kutoka sharika wanazosali, na pia huwapa nafasi ya kusimama na kujitambulisha wenyewe wasiokuwa na barua hizo.
Badala ya kusalimia kwa Neno la Mungu kama ‘Bwana Yesu asifiwe, tumsifu Yesu Kristu’ au kusema ‘Haleluya’, kisha akajitambulisha na kuketi ili asimame mtu mwingine, yeye alitumia mwanya huo kuwaomba Walutheri nchini wamchague kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa vile naye ni Mlutheri!
Aliomba wamuombee kwa sala zao zote ili dhehebu hilo nchini nalo litoe rais, ujinga ambao wananchi hawakutarajia kama ungeweza ukafanywa na mgombea wa nafasi hiyo muhimu kwa taifa!
Lakini bila wasiwasi wala aibu usoni, Mbatia alijitokeza hadharani, mbele ya kamera za televisheni kadhaa nchini kumtetea Lowassa kwa kupotosha waziwazi.
Alidanganya, kwamba alichosema eti ni kuomba aombewe ili ashinde siku ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwezi ujao, jambo linalofanywa na kila mmoja anayegombea nafasi yoyote ile ya madaraka ya kisiasa wakiwemo hata washirikina.
Sitaki kuamini kuwa Mbatia ni muongo sana, mzushi sana, zuzu sana, tapeli wa kisiasa, mvivu wa kufikiri, mpotoshaji mkubwa na hata vinginevyo, lakini imebidi nimtathimini kwa kutumia sifa hizo ili kupata undani wake.
Hata kwa akili ya kawaida ni je, hivi ni kweli Lowassa aliposema ‘nyie Walutheri mna sababu ya kuomba zaidi kwa sababu tangu nchi hii iumbwe haijapata Rais Mlutheri’, maneno aliyoyasema mwenyewe alikuwa eti anaomba aombewe ushindi na Walutheri hao?
Je, ni kweli kwamba alipotolea mfano wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa kusema wote walikuwa Wakatoliki, huyo alikuwa anaomba aombewe ushindi kwa sababu za kawaida za imani yake Kiroho?
Au Lowassa aliposema kwamba ‘Sasa nadhani Mungu atatuongoza ili nasi (Walutheri) tuweze kuipata nafasi hiyo (ya urais)’, alikuwa akiomba, kwamba aombewe kwa taratibu za kawaida na siyo kwa sababu ni Mlutheri?
Ni kweli kuwa kwa maneno yake hayo, kauli zake hizo na hata vinginevyo alikuwa akitaka aombewe ushindi?
Nimesema sitaki kuamini kuwa Mbatia ni tapeli wa kisiasa, muongo sana, mzushi, mpotoshaji na kadhalika, lakini nina haki ya kutilia wasiwasi uwezo wake wa kufikiri, uadilifu wake na hata ubora wake wa kuongoza watu akiwa mbunge au Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Siasa.
Ni vigumu katika hali ya kawaida hasa kwa mtu asiyehongwa, kiongozi mwadilifu na anayejua na kuthamini ukweli kupata ujasiri ulioonyeshwa na Mbatia wa kwenda kutetea upuuzi na tena hadharani!
Najaribu kutafakari endapo kweli ni adui mkubwa wa watuhumiwa wa wizi wa fedha za serikali, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Najiuliza kwa sababu siamini kuwa Mbatia, aliyekuwa mmoja kati ya vinara wa kukemea ufisadi, mafisadi wenyewe au wanasiasa na watumishi wa umma wenye tuhuma hizo za jinai hivi sasa ndiye wakili wao mkubwa.
Najiuliza sana kama sasa ni mmoja kati ya viongozi wa kisiasa wanaohongwa sana, kwamba inawezekana akawa tayari amehongwa kwa namna moja ama nyingine ili awe mstari wa mbele kujibu tuhuma zote, kutetea maovu yote na upuuzi wote wa kisiasa unaofanywa na mgombea huyo wa urais wa Chadema.
Ni vigumu katika hali ya kawaida kupata ujasiri mkubwa kiasi hicho, ule ambao umeshindikana kwa Lowassa mwenyewe, familia yake, Chadema yenyewe na hata washauri wake wa karibu, badala yake umekuwa ukifanywa na Mbatia, ambaye hana uhusiano naye wowote.
Najiuliza kuwa kwa nini wakati Lowassa alipotuhumiwa na Dk. Slaa kuwa fisadi, bila kujifichaficha na hata vinginevyo, alijitokeza hadharani na haraka ili 'kumkingia kifua' kwa Watanzania?
Najiuliza sana ilikuwaje afikie mpaka hatua ya kutaka eti mafisadi wasamehewe, msimamo ambao unatia shaka endapo ulikuja kwa utashi wake mwenyewe ama la.
Najiuliza sana kama hafanyi hivyo kwa sababu amehongwa fedha za Lowassa mwenyewe, wapambe wake, Chadema yenyewe au kundi lolote ili afanye kazi hiyo isiyowezekana kwa 'macho makavu'.
Ili aweze kuniondolea mashaka ya wingu hilo dhidi yake, Mbatia anaweza kutuambia kuwa ni nani hafahamu Kiswahili mpaka ashindwe kuijua kauli ile ya Lowassa kanisani na kudai eti hakueleweka?
Au, kama siyo msemaji rasmi wa mgombea huyo wa urais, Mbatia anaweza kutuambia kuwa analinda maslahi gani kwa Lowassa?
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

No comments:

Post a Comment