Sunday, 27 September 2015

SAMIA: DK. MAGUFULI KIBOKO YA MIGOGORO




NA KHADIJA MUSSA, MVOMERO
MGOMBEA Mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema mwarobaini wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima anao mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, hivyo aliwataka wananchi wa Mvomero kumchagua.
Amewataka wasikubali kubabaishwa na wapinzani wanaopita katika maeneo yao na kudai kuwa wana uwezo wa kumaliza migogoro inayowakabili kwa vile ni waongo kwani hawana hata mipango ya  kutatua migogoro hiyo.
Samia alisema CCM ndicho chama pekee chenye uwezo na dhamira ya dhati ya kutatua changamoto mbalimbali  zinazowakabili katika maeneo yao, ambapo utekelezaji wake umeainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika kata ya Mailimoa kwenye eneo la Kipera, jimboni Mvomero, juzi, Samia alisema hakuna mwenye uwezo wa kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji zaidi ya serikali ya CCM.
Mvomero ni moja ya maeneo ambayo yanakabiliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi kutokana na baadhi ya watu kujimilikisha mashamba makubwa bila ya kuyaendeleza na kuwaacha wakulima na wafugaji wakikosa maeneo ya kufanya shughuli zao.
Samia alisema wanatambua changamoto hiyo na tayari mikakati ya kuzitatua imeshapangwa, ambapo Dk. Magufuli akichaguliwa kuwa rais, moja ya kipaumbele vyake ni kushughulika na maeneo ambayo hawajayaendeleza, hivyo wananchi hao wanatakiwa kuhakikisha wanapiga kura nyingi kwa CCM siku itakapofika.
"Ndugu zangu wa Mvomero matatizo ya ardhi yanayosababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji tayari yameshapatiwa dawa, hivyo nawaomba mumchague Dk. Magufuli katika nafasi ya urais na Sadiq Murad kuwa mbunge na madiwani wote wa CCM, kwani ushirikiano huo kwa kuongozwa na Ilani, tatizo hili litakuwa historia," alisema.
Awali, wananchi hao walimuomba Samia kuwasaidia katika ujenzi wa soko la kisasa pamoja ujenzi wa barabara ya Mzumbe-Mlali, Mgeta -Nyandili kwa kiwango  cha lami, ambapo alisema masuala hayo yote yatatekelezwa kupitia ilani kwa kuwa yote yameainishwa.
Kwa upande wake, Murad alisema atahakikisha Dk. Magufuli anashinda kwa asilimia zaidi ya 80, kutokana na jimbo hilo kuwa ngome ya Chama.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa maji safi na salama kwani licha ya kuchimba visima, bado havijatosheleza mahitaji ya wananchi wa jimbo ambapo alimuomba serikali ijayo kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Samia alisema tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini atahakikisha analishughulikia mwenyewe kwa kuwa anajua adha waipatayo kinamama wanapotembea umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kutafuta maji.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogeries, aliwataka wananchi hao kupuuza kelele za wapinzani kwa kuwa hazina tija, badala yake wajitokeze kwa wingi siku ya kupigakura itakapofika na kuchagua wagombea wa CCM katika nafasi zote, ikiongozwa na ya urais.
Karogeries alisema wananchi hao wasihadaike na baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM waliojiunga na UKAWA, ambao aliwafananisha na kupe kwa sababu ng'ombe akiwa na kupe, kazi yao ni kunyonya damu na anapouzwa lazima ataambatanao.
Alisema Tanzania hakuna mgombea urais mwenye uwezo mkubwa kiutendaji, mzalendo na muadilifu zaidi ya Dk. Magufuli, hivyo siku ya kupiga kura itakapofika, wahakikishe kura zote za urais zinakwenda kwake, wabunge na madiwani wa CCM.

No comments:

Post a Comment