Na Chibura Makorongo,Shinyanga
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John
Magufuli, amempongeza mgombea ubunge wa jimbo la Solwa, Ahmed Salum, kwa
kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Dk. Magufuli alitoa pongezi hizo
juzi, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jimbo la Solwa, katika moja ya mikutano
yake ya kampeni, uliofanyika kijijini Solwa.
Mgombea huyo wa urais wa CCM
aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kuhakikisha wanamchagua tena
Salum ili aendeleze miradi ya
maendeleo aliyokwishaianzisha.
Alisema binafsi anamfahamu Salum kuwa
ni mmoja wa wabunge wenye upeo mkubwa katika ufuatiliaji wa mambo na
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Ndugu zangu wakazi wa Solwa,
tumekuja hapa kuwaombeni kura zenu Oktoba 25, mwaka huu, msifanye makosa,
nichagueni mimi Magufuli, kwa ubunge mpigieni jembe lenu, Ahmed (Salumu) na
madiwani wote wa CCM, msifanye makosa, tunataka funguo tatu, msituchanganyie
vyama,” alisema.
Akielekezea mafanikio ya utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi katika jimbo hilo, Salum alisema moja ya mambo aliyoyafanyia
kazi ni usambazaji wa huduma ya maji na umeme katika maeneo mengi ndani ya
jimbo lake, ikiwemo uboreshaji wa elimu.
Salum alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, alikamilisha mradi wa maji ya bomba katika vijiji vya Ng’homango, Kadoto, Jimondoli, Ichogo, Lyabusalu na Mwajiji, ambao umewezesha watu 212,710 kupata maji safi na salama, uliotekelezwa kwa fedha iliyotolewa na serikali kuu.
“Mheshimiwa mgombea urais, ndani ya
miaka mitano nimefanya mengi, lakini kwa upande wa sekta ya maji ninatarajia
ifikapo Desemba, 2015, idadi ya wananchi watakaopata huduma ya maji safi na
salama itaongezeka kutoka asilimia 60.03 ya sasa hadi asilimia 68.52 baada ya
vijiji vingine vinane kupatiwa huduma hiyo,” alisema.
Kuhusu miundombinu ya barabara,
alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga, imefanikiwa kuongeza mtandao wa barabara na kufikia kilometa
1,239.89, ikiwa ni pamoja na kukarabati maeneo korofi kwa kutumia fedha kutoka
mfuko wa barabara.
00000
No comments:
Post a Comment