Sunday, 27 September 2015

RIDHIWANI AAHIDI UMEME VIJIJINI




Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Chalinze kupitia CCM, Ridhiwani Kikwete, amesema iwapo atachaguliwa kuongoza jimbo hilo, atahakikisha anapeleka umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa pamoja na kwenye Zahanati ya Lupungwi na Kata ya Mandera.
Alisema awamu ya kwanza ya utawala wake, Wakala wa Umeme Vijijini (REA), walipeleka nguzo za umeme 120, lakini mkandarasi aliyekuwa anasimamia mradi huo alidai vifaa alivyonavyo ni kwa ajili ya nguzo 60. 
Ridhiwani alisema hivi sasa nguzo zimepatikana na umeme umeanza kuvutwa kwa kuwekwa nyaya kuanzia Makole- Mungu, Yatosha-Lupungwi hadi Kimange. 
Alisema iwapo atachaguliwa, atahakikisha anaendelea kusimamia mipango ambayo imeanzishwa na kutekeleza miradi iliyobaki ili kuondoa changamoto mbalimbali.
Akizungumzia barabara ya Lupungwi hadi Miono, alisema dhamira yake ni kuiunganisha barabara hiyo ili kukutanisha vijiji na vitongoji na makao makuu ya kata.
Mgombea udiwani wa Kata ya Mandera, Madaraka Mbode, alisema endapo atachaguliwa, atahakikisha anashirikiana na mbunge kutatua tatizo la umeme katika kijiji cha Lupungwi na kujenga kituo cha afya katika kata ya Mandera na Zahanati ya Kibaoni.

No comments:

Post a Comment