“MOJA, mbili, tatu, nne… tano,” ni maneno ya Watanzania
kwenye moja ya mikutano ya kampeni iliyofurika umati mkubwa wa watu walipokuwa
wakihesabu idadi ya ‘push-up’ zilizopigwa na Dk. John Magufuli, mgombea urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM.
Kumalizika kwa ‘push-up’
hizo kulifuatiwa na nderemo, vifijo na makofi ya kutosha kutoka kwa maelfu ya
watu waliohudhuria mkutano huo.
Huku akishangiliwa muda
wote alipokuwa akipiga ‘push-up’ hizo, Dk. Magufuli alionyesha dhahiri kwamba
yuko fit’ kiakili, kifikra, kimwili na kiafya.
Wengi waliendelea kupiga
kofi na kushangilia kwa nguvu baada ya kumuona kiongozi na kipenzi chao akifanya
mazoezi hayo ya viungo jukwaani tena kwa kujiamini.
Kwa kawaida michezo huleta
furaha, amani, faraja, afya ya akili na mwili. Kuna tofauti moja kubwa baina ya
viongozi wengi wa Afrika dhidi ya wale wa nchi za magharibi, zikiwemo Uingereza
na Marekani.
Waafrika wengi wawapo
madarakani hunenepa na kuota vitambi na wakati mwingine huandamwa na maradhi
yatokanayo na unene. Kinyume chake wazungu wengi wawapo madarakani miili yao
huwa miembamba kwa sababu ya kutenga muda wa kushiriki michezo pamoja na
mazoezi ya viungo.
Arnold Schwarzenegger ni
mwanasiasa na kiongozi mashuhuri nchini Marekani. Anajulikana kwa filamu zake za
kusisimua ikiwemo filamu maarufu ya Komando. Licha ya umri wake kusonga, bado Arnold
ni mkakamavu na mwenye afya imara.
Nelson Mandela, rais wa
kwanza mweusi wa taifa la Afrika Kusini na mtu mashuhuri kabisa duniani,
alikuwa mwanamichezo imara na mtu wa mazoezi. Mandela alikuwa mwanamasumbwi
hodari na aliwatoa nishai wapiganaji maarufu wa masumbwi nchini humo.
Licha ya siasa za ubaguzi
wa rangi kushamiri nchini humo, bado Mandela alionyesha uwezo mkubwa kwenye
mchezo huo wa masumbwi huku akiwalambisha mchanga mabondia wengi maarufu
wakiwemo wa nje ya nchi hiyo. Mungu alimjalia shujaa huyo wa Afrika Kusini afya
njema na maisha marefu.
Pamoja na baraka hizo za Mungu,
michezo na mazoezi ya viungo navyo vilichangia kwa kiasi kikubwa kumpa Mandela
afya imara pamoja na ukakamavu wa kiakili, kifikra, kiafya na kimwili.
Barak Obama, rais wa
Marekani kutoka taifa lenye nguvu zaidi kuliko yote duniani, ni mwana michezo
mahiri na kitendo chake cha kufanya mazoezi pamoja na kushiriki kwenye mchezo aupendao
wa kikapu, imemfanya apendwe na kuheshimika zaidi katika jamii ya Wamarekani.
Obama ni mmoja wa viongozi wanaopendwa sana duniani. Sina shaka kupendwa na
kukubalika kwake huko kunatokana na uwezo mkubwa wa uongozi alionao.
Vilevile, Obama ana kipaji
kikubwa sana cha kuongea, kushawishi na kujenga hoja. Pia rais huyo mwenye
asili ya Kenya ni kiongozi aliyejaliwa akili, maarifa na werevu wa kila aina.
Naamini kabisa kwamba mafanikio
ya kisiasa na kidiplomasia aliyonayo Obama yanatokana na baraka za Mwenyezi
Mungu, uadilifu, uchapakazi, kujishusha kwake na mazoezi ya viungo, ambayo huyafanya
kila siku asubuhi na jioni.
Mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM Dk. John Magufuli ni mwanamichezo na mtu
wa mazoezi kwelikweli. Mazoezi hayo ambayo amekuwa akiyafanya kwa miaka mingi,
yamegeuka kuwa sehemu ya utamaduni wake wa kila siku.
Kitendo cha Dk. Magufuli
cha kupiga ‘push-up’ tano ni ujumbe tosha kwa Watanzania kwamba, pindi
atakapokuwa rais wa nchi yetu, atapenda kuona Watanzania wanakuwa wachapakazi
na kwamba ili uwe mchapakazi, ni lazima uwe mkakamavu. Hakuna njia nyingine ya
kuwa mkakamavu zaidi ya kufanya mazoezi ya viungo.
Ujumbe mwingine anaotoa Dk.
Magufuli kupitia ‘push-up’ zake umejielekeza katika kuwaeleza Watanzania kwamba
ukakamavu hauishii kwenye uimara wa mwili au afya pekee, bali unavuka mipaka na
kugusa maeneo mengine muhimu yanayomhusu binadamu. Maeneo hayo ni pamoja na
ukakamavu wa kielimu, kifikira na kimtazamo.
‘Push-up’ za Dk. Magufuli
zinabeba ujumbe kwamba jukumu la urais kwa maana ya uongozi wa nchi ni zito na
linahitaji afya imara. Kadhalika uimara wa afya hauishii kwa rais pekee bali
kwa watendaji, viongozi na wasaidizi wengine wa rais.
Uimara wa afya za viongozi
ikiwemo afya ya rais wa nchi inatokana na ukweli kwamba uongozi ni mapambano ya
kufa na kupona yanayohitaji nguvu ya akili, nguvu ya maarifa, nguvu ya
kustahimili mambo mazito pamoja na nguvu za mwili. Kila jambo zito linaloikabili
nchi au jamii husika humhusu moja kwa moja kiongozi wa eneo husika.
Rais Obama alipoingia
madarakani mwaka 2008, alikuwa mtanashati na kijana maridadi kabisa. Obama wa
sasa kabadilika huku dalili za uzee zikianza kumwandama. Sababu kubwa ni uchovu
unaotokana na uzito wa majukumu ya urais. Nelson Mandela alihudumu nafasi ya
urais kwa muhula mmoja tu wa miaka mitano na kulazimika kustaafu kwa sababu za
kiafya na uzee.
Ujumbe mwingine anaoutoa
Magufuli ‘Tingatinga’ kupitia ‘push-up’ zake hizo ni kwamba endapo atachaguliwa
kuwa rais wa nchi hii, ataimarisha sekta ya michezo na sanaa kwa kujenga na
kuimarisha miundombinu ya michezo nchini, kupanua wigo wa vyanzo endelevu vya
fedha za uendeshaji na ugharamiaji wa maendeleo ya michezo hapa nchini kwa kuanzisha
Bahati Nasibu ya Michezo; kuhamasisha na kusisimua maendeleo ya michezo katika
ngazi zote hapa nchini kwa kuendeleza matamasha ya michezo kuanzia ngazi za
vijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa.
Aidha, ujumbe wa ‘push-up’
za Dk. Magufuli unaonyesha dhamira yake ya kuweka vivutio vya kuwavutia
wawekezaji na washiriki wengine kuwekeza na kugharamia shughuli mbalimbali za
michezo nchini.
Kwa upande mwingine, mazoezi
kabambe ya ‘push-up’ za Dk. Magufuli ni kielelezo dhahiri cha jinsi alivyopania
kuboresha tasnia ya sanaa ikiwemo filamu, muziki na michezo ya kuigiza.
Vijana wengi walimshangilia
sana Dk. Magufuli kwa ‘push-up zake. Sidhani kama walielewa hasa maudhui ya ‘push-up’
hizo. Kwa faida ya vijana wenzangu, Dk. Magufuli anatutaka tusiwe wavivu, wazembe
na wababaishaji. Kinyume chake tuwe wakakamavu katika kuilinda nchi yetu.
Ukakamavu wetu uonekane na kila mtu, yakiwemo maslahi mapana ya ulinzi wa amani
ya nchi yetu dhidi ya maadui wa ndani na wa nje.
Dk. Magufuli anatufundisha
kwamba atafurahi sana kutuona vijana tukiwa wakakamavu zaidi kuliko yeye. ‘Push-up’
tano zinaashiria kwamba awamu ya kwanza ya miaka mitano ya urais wa Magufuli
itatawaliwa na uchapakazi wa kiwango cha hali ya juu. Kadhalika, awamu ya pili
ya miaka mingine mitano ya urais wake, itatawaliwa na uchapakazi wa kiwango cha
hali ya juu zaidi!
Fahari na faraja ya Watanzania
ni kuona Dk. Magufuli anakuwa rais wa awamu ya tano wa nchi yetu.
Mwandishi wa makala hii ni
Amos Siyantemi
0655689461
0754689461
No comments:
Post a Comment