Wednesday 8 June 2016

CHINA YAITANGAZIA NEEMA TANZANIA


SERIKALI ya China kupitia Benki ya Exim, imesema ipo tayari kushirikiana na Tanzania, kutekeleza  miradi mikubwa, ukiwemo wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge).

Pia, imeahidi kuendelea kuisaidia serikali ya awamu ya tano katika malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili viweze kuzalisha asilimia 40 ya ajira hapa nchini.

Ahadi hiyo ilitolewa jana, Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Zhang Shuo, alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Aziz Mlima.

Zhang alisema benki yake tayari imeidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, kama vile ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, Kisiwani Unguja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Dar es Salaam–Chalinze hadi Arusha, yenye uwezo wa kusafirisha kilowati 400.

Alisema Exim imeanzisha mfuko maalumu wa kusaidia  maendeleo ya viwanda barani Afrika, ambao umetengewa Dola za Marekani bilioni 10 (takriban sh.trilioni 21.90), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais wa China, Xi Jinping, aliyoitoa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na China, uliofanyika Afrika Kusini, Desemba, mwaka jana.

"Tanzania itakuwa ni moja ya nchi zitakazonufaika na fedha za mfuko huo, ambazo pamoja na mambo mengine, imepanga kuzitumia kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu wezeshi ya barabara, reli na umeme kwenye Eneo la Uwekezaji (EPZA), wilayani Bagamoyo, Pwani,"alisema.

Zhang alisema lengo la ziara yake hapa nchini ni kujadili masuala ya kiufundi na wadau mbalimbali ili utekelezaji wa miradi inayokusudiwa uanze haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa Zhang, amefurahishwa na ziara hiyo kwa kuwa wadau wote aliokutana nao wameonyesha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa miradi husika.

Kwa upande wake, Dk. Mlima aliishukuru China kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais, Dk. John Magufuli ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Dk. Mlima aliahidi ushirikiano wa wizara yake na serikali kwa ujumla ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi bila vikwazo.

Benki ya Exim ya China, imeshatoa mikopo mbalimbali kwa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ujenzi wa vinu vya kuzalisha umeme wa Kinyerezi III na IV.

No comments:

Post a Comment