TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi sh. bilioni 12 kwa Rais Dk. John Magufuli, zilizobaki baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais, uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alikabidhi hundi ya fedha hizo kwa Rais Magufuli jana, jijini Dar es salaam na kueleza kuwa, bakaa ya fedha hizo haikuathiri kwa namna yoyote uchaguzi huo.
"Mheshimiwa Rais, fedha ambazo tunakukabidhi, tulijibana sana, japo muda wenyewe ulikuwa mfupi, lakini tulijibana bila kuathiri utendaji wa shughuli za uchaguzi. Isije ikawa inatoa sura kwamba iliathiri chochote, la hasha. Katika hali hiyo, kama ambavyo wengi ni mashahidi, hatujisifu, lakini uchaguzi ulikwenda vizuri,"alisema Jaji mstaafu Lubuva.
Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais Magufuli aliipongeza NEC kwa kuokoa fedha hizo na kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine, ambapo ametaka taasisi zingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa.
"Kitendo hiki ambacho mmekionyesha leo, kinaonesha ni kwa namna gani Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya uongozi wako mwenyekiti, ilivyo na watu makini na waadilifu sana. Kwa sababu hizi fedha, ambazo kwa lugha uliyotumia ni bakaa, kutokana na zile ambazo mlipewa zaidi ya shilingi bilioni 270, mkatumia shilingi bilioni 261.6, mkabakiza shilingi bilioni 12, mngeweza kuamua kusema hamkubakiza na hakuna mtu yeyote ambaye angekuulizeni.
"Pengine hakuna mtu yeyote, ambaye angejua na kusema kiasi mlichotupa hakijatosha. Tunaomba mtuongezee ama mngetengeneza maneno mazuri ya matumizi, bado nina uhakika serikalini wasingejua,"alisema Rais Magufuli.
Pamoja na kukabidhi hundi hiyo, Jaji Lubuva alimuomba Rais Magufuli aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi kwa kuwa hivi sasa, NEC inatumia majengo ya kupanga, ambayo yanaigharimu takribani sh.bilioni 1.400, kila mwaka, kwa ajili ya kulipia kodi ya pango, usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.
Rais Magufuli alikubali ombi hilo na kuamua kuwa, fedha hizo zilizorudishwa na NEC, zitumike kujenga ofisi yake na kupendekeza ofisi hiyo ijengwe mkoani Dodoma.
"Na mimi ningefurahi zaidi kama hilo jengo lingejengwa Dodoma, kwa sababu Dodoma ndio makao makuu ya nchi hii na hasa kwa sababu Dodoma ni katikati ya Tanzania,"alisisitiza Rais Magufuli.
Dk. Magufuli pia alikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa kwa mfuko wa tume ya uchaguzi, ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata, badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za kugharamia uchaguzi husika.
No comments:
Post a Comment