Wednesday, 8 June 2016

MAJALIWA: MPANGO WA MAENDELEO KUBORESHA AJIRA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017-2020/2021, unalenga kuboresha maisha ya Watanzania wengi kwa kuhakikisha sekta zinazoajiri watu wengi na walio masikini zinakuwa kwa kasi.

Akizindua mpango huo jana, katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, mjini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali itahakikisha sekta za kilimo, viwanda, uvuvi na mifugo zinakua kwa kasi ya kuridhisha ili kuongeza fursa za ajira na kupunguza umasikini.

Majaliwa alisema utekelezaji wa mpango huo, ambao umefungamanisha maendeleo ya viwanda na yale ya watu, unatazamiwa kujibu changamoto ya umasikini hapa nchini.

Waziri Mkuu alisema maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika mpango huo ni miradi mikubwa kama ya chuma cha Liganga, kufufua shirika la ndege, makaa ya mawe ya Mchuchuma, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha 'standard gauge', ambayo matokeo yake yanatarajiwa kuwa kichocheo cha utekelezaji wa miradi mingine.

“Tunatarajia ifikapo mwaka 2025, tuwe tumejenga nchi ambayo ina maisha bora, yenye amani, umoja na utawala bora, jamii inayojifunza na iliyoelimika, yenye uwezo wa kuzalisha na kuwa na ukuaji wa uchumi endelevu na wenye ushindani,”alisema.

Majaliwa alisema azma ya serikali ni kuhakikisha ukuaji huo wa uchumi unakuwa shirikishi zaidi katika utekelezaji wa mpango huo na kwamba, uendelezaji wa viwanda ndiyo utakaoleta mafanikio makubwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa alisema jumla ya viwanda 39 kati ya 106, vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ambavyo vilikuwa vinazalisha bidhaa za chuma, ngozi, korosho zana za kilimo, sabuni na mafuta ya kupikia vilifungwa kutokana na kutoendelezwa.

Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kwa Msajili wa Hazina, itaendelea kuvirejesha serikalini ili uangaliwe utaratibu mwingine ulio bora wa kuviendeleza kupitia mpango huo.

Alisema mpango huo utajikita zaidi katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza viwanda vikubwa, vya kati na vidogo na vile vilivyobinafsishwa, ili kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi wengi.

Akizungumzia utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, ambao utahitimishwa Juni 30, 2016, alisema serikali ilifanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara za lami na madaraja ya Kigamboni, Maligisu Nagoo, Mbutu na Ruhekei.

Pia, alisema serikali ilifanikisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, lenye urefu wa kilomita 542, ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi katika maeneo ya Madimba na Songosongo, ujenzi wa vituo vya kupokelea gesi vya Somanga-Fungu na Kinyerezi.

No comments:

Post a Comment