Wednesday, 8 June 2016
MAFUNDI GEREJI WATENGENEZA BURE MAGARI YA SERIKALI, WACHANGIA MADAWATI 100
UMOJA wa Mafundi Magari Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, (Magereji Tegeta), umemkabidhi magari manne ya serikali, Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda baada ya kuyafanyia matengenezo makubwa, ikiwa ni hatua ya kusaidia na kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Dk. John Magufuli.
Pia, umoja huo umekabidhi mchango wa madawati 100, kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto ya madawati kwa shule mbalimbali mkoani humo.
Magari yaliyokabidhiwa jana ni kati ya magari manane kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, yaliyokuwa mabovu na inadaiwa yalikuwa katika harakati za kuuzwa kwa baadhi ya vigogo kwa bei nafuu.
Umoja huo uliamua kuyaachukua magari hayo na kuyatengeneza kwa gharama zao, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono harakati za serikali ya mkoa na serikali kuu, kwa kuwawezesha watendaji wa idara mbalimbali kuwahudumia wananchi.
Akipokea magari na madawati hayo, Makonda aliupongeza umoja huo na kusema, umeandika historia ya kipekee kwa hatua hiyo kubwa.
“Sijawahi kusikia mafundi gereji duniani, waliotengeneza magari ya serikali yao. Hata watumishi walioko ndani ya mkoa wangu, walikuwa wanasubiri jambo hili likwame na wengine walikuwa wanasubiri vifaa viibwe, kwa sababu walikwishaweka utamaduni wa kujiuzia magari kwa bei nafuu, hivyo walikuwa wakisubiri kujiuzia,”alisema.
Aliongeza: “Haiwezekani gari ambalo umekataa kulitumia kiofisi kwa shughuli za serikali kwa kudai ni bovu, halafu unapolinunua, unalitumia binafsi na kuingia nalo ofisini. Ninyi mmenipa ujasiri wa kuandika neno hapana.”
Alisema kutokana na hatua hiyo, hawezi kumvumilia mfanyakazi yeyote, ambaye atabaki na kuzunguka ofisini badala ya kutoka kwenda kuwahudumia wananchi.
"Kwa kutengeneza magari hayo ya serikali bure, umoja huo umeondoa sababu ya watendaji kubaki ofisini,"alisema.
Alisema wapo watu, ambao walikwishaweka oda ya kujiuzia na kuyanunua magari hayo kwa bei chee, kutokana na utamaduni wa kujiuzia mali za serikali kwa bei ya kutupa.
Aidha, Makonda aliushukuru umoja huo kwa machango wa madawati 100, ambayo alisema yatasaidia kupunguza changamoto kwa wanafunzi mkoani humo.
Akikabidhi magari hayo, Mwenyekiti wa Umoja wa Magereji Tegeta, Alawi Kassimu, alisema magari hayo manne, yametengenezwa kwa awamu ya kwanza, ambapo awamu ya pili yatatengenezwa mengine yaliyosalia, ambayo hakutaja idadi yake.
Alisema umoja huo unatambua kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya tano, hivyo waliona kuna umuhimu wa kusaidia katika kutengeneza magari hayo pamoja na kutoa msaada wa madawati hayo 100.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment