SERIKALI imetenga sh. trilioni 11,820.503, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ili kutekeleza miradi ya maendeleo katika mwaka 2016-2017.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango, alipowasilisha taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016-2017.
Dk. Mpango alisema katika bajeti hiyo, fedha za ndani ni sh. trilioni 8,702.697, sawa na asilimia 74 ya bajeti ya maendeleo na fedha za nje ni sh. trilioni 3,117.805, sawa na asilimia 24 ya bajeti ya maendeleo.
Alisema sekta binafsi inatarajiwa kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha ili kuanzisha na kuendeleza viwanda, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango.
Dk. Mpango alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016-2017, umegawanywa katika makundi manne, ambayo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda.
Makundi mengine ni kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na usimamizi wa utekelezaji wa mpango.
Alisema kwa upande wa viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni mradi wa magadi soda- Bonde la Engaruka Arusha, mradi wa kufufua kiwanda cha General Tyre Arusha, uendeshaji wa viwanda vidogo-SIDO katika maeneo ya viwanda ya Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro.
Dk. Mpango alisema miradi itakayotekelezwa katika eneo fungamanishi na maendeleo ya uchumi na rasimali watu ni kuimarisha mifumo, majengo na miundombinu katika shule za awali, msingi na sekondari.
Miradi mingine ni upanuzi na ujenzi wa vyuo vikuu vya ualimu na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi, kuboresha hospitali za rufaa, Taasisi ya Saratani Ocean Road na hospitali ya magonjwa ya kuambukiza Kibong'oto.
Kwa upande wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji, Dk. Mpango alisema serikali itaendelea kutekeleza miradi iliyoanza kutekelezwa katika kipindi cha Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano.
Waziri huyo alisema katika mwaka 2016-2017, serikali itaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango kwa lengo la kurekebisha upungufu uliojitokeza katika utelekezaji wa mpango wa programu mbalimbali za maendeleo.
Dk. Mpango aliitaja miradi mikubwa ya kielelezo, itakayopewa msisitizo katika utekelezaji wake kuwa ni pamoja na kununua ndege tatu mpya, moja ikiwa ni Bombardier CS300, yenye uwezo wa kubeba abiria 100 hadi 150 na ndege mbili aina ya Bombardier Q400, zenye uwezo wa kubeba abiria 67 hadi 88 kila moja.
Miradi mingine ni ujenzi wa reli mpya ya kati kutoka Dar Salaam- Kigoma- Tabora-Mwanza, ununuzi wa meli moja mpya ya kusafirishia abiria na mizigo katika Ziwa Victoria, Mv Butiama na MV Liemba, mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na mradi wa chuma Liganga.
Akizungumzia mwelekeo wa uchumi 2016-2017, Dk. Mpango alisema shabaha na malengo ya uchumi kwa ujumla ni kukua kwa pato halisi la taifa kwa asilimia 7.2 mwaka 2016 kutoka 7.0 mwaka 2015.
Mwelekeo mwingine ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa, unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 ya asilimia 8.0 mwaka 2016.
Mengine ni mapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 14.8 ya Pato la Taifa, mwaka 2015-2016 na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.9 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2016-2017. Aidha, mapato ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016-2017 kutoka asilimia 12.6 ya Pato la Taifa mwaka 2015-2016.
Aidha, Dk. Mpango alisema matumizi ya serikali yanatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 23.2 ya Pato la Taifa mwaka 2015-2016 hadi asilimia 27.0 mwaka 2016-2017.
Alisema nakisi ya bajeti inatarajiwa kuwa asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016-2017, kutoka makadirio ya bajeti ya asilimia 4.2, mwaka 2015-2016.
Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida kuwa asilimia 7.9 ya Pato la Taifa mwaka 2015-2016 na kupunguza hadi asilimia 7.5 mwaka 2016-2017. Pia kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne ifikapo Juni, 2017.
Dk Mpango aliitaja miradi iliyokamilika mwaka 2015-2016, kuwa ni ujenzi wa madaraja ya Kigamboni, Maligisu, Nangoo, Mbutu na Ruhekei katika barabara kuu.
Mingine ni ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, urefu wa kilometa 542 na ujenzi wa mitambo ya kuchakachua gesi katika maeneo ya Madimba na Songosongo.
Miradi mingine ni ujenzi wa vituo vya kupokea gesi vya Somanga-Fungu na Kinyerezi, usimikaji wa mitambo minne ya kufua umeme Kinyerezi 1, yenye uwezo wa kuzalisha MW 150 na kuanza uzalishaji wa umeme.
Mingine ni awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA) na kuunganisha wateja 61,023, wa awali kati ya wateja 250,000. Pia kukamilika kwa awamu ya Pili ya Mkongo wa Taifa wa mawasiliano (kilometa 25,954) na kusambazwa katika mikoa 24 ya Tanzania Bara.
Miradi mingine ni kukamilika kwa mradi wa maji wa Ruvu Chini (Pwani) na kukamilika kwa miradi mipya ya 1,160 ya maji ya vijiji 10, katika vijiji 1,206, yenye vituo 28,499 vya kuchotea maji katika Halmashauri 148.
No comments:
Post a Comment