Wednesday, 8 June 2016

NASSARI, MADIWANI WANNE CHADEMA WASAKWA NA POLISI


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassary pamoja na madiwani  wanne wa chama hicho, wanasakwa na polisi mkoani hapa kwa kosa la kuvunja masharti ya dhamana ya polisi.

Mbali na hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru wilayani Arumeru mkoani hapa, Willy Njau na madiwani  wenzake 23, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kujibu shitaka la kuharibu mali kwa makusudi.

Akizungumza na Uhuru, jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema Mei 8, mwaka huu, Nassary na madiwani 29 walipewa dhamana katika kituo cha polisi cha Usa River, walipokuwa wanashikiliwa kwa kosa la kuvunja uzio wa kiwanja na kuharibu mali kwa makusudi.

Alisema baada ya dhamana hiyo, Nassary na wenzake walitakiwa kufika kituo cha polisi cha Usariver,  Juni 8, mwaka huu, kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo, lakini hawakutokea.

“Kutokana na Nassary na wenzake, ambao ni Paulo Samwel, Japhet Joseph, Zefania Mango na Anderson Elisarikawa, kukiuka masharti ya dhamana, tunawasaka popote walipo hata kama ni Dodoma ili tuwaunganishe kwenye kesi inayowakabili,”alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru,Wilayani Arumeru mkoani hapa, Willy Njau na madiwani wenzake 23, walipandishwa kizimbani jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kujibu shitaka la kuharibu mali kwa makusudi.

Akisoma shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augustino Rwizile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Timothy Vitalis, alidai washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Mei 4, mwaka huu, eneo la Leganga, Usa River wilayani humo.

Vitalis alidai mahakamani hapo kwamba, washitakiwa hao walivamia kiwanja mali ya mfanyabiashara Itandumi Makere, kuvunja uzio na kuharibu mali zenye thamani ya sh.7,000,000, kwa makusudi huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, watuhumiwa wote walikana shitaka hilo, ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi  Juni 28, mwaka huu. Washitakiwa wote wako nje kwa dhamana ya sh.2,000,000 kila mmoja.

Katika hati hiyo ya mashitaka, iliyowasilishwa mahakamani hapo,  Nassary ni mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo.

Washitakiwa  wengine ni Nelson Wilium, Elisa Steven, Nelson Mafie, Wilson Fanuel, Digna John, Roman Laurence, Josephine Anael, Samwel Ismail, Agness Eliya, Izack Afito na Neema Izach.

Wengine ni Gadiel Stanley, Jeremia Masawe, Peter Efatha, Bernad Wilson, Hendry Benjamin, Emanuel pendael, Fadhila Joseph, Penzila Palangyo, Merry Anton, Eveline Julius, Bryson Mosses na Frank Ngoye.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Paul Wiliam, anaripoti kutoka mkoani Kilimanjaro, kwamba, polisi inamshikilia Mbunge wa Jimbo la Siha mkoani humo, Dk Godwin Mollel (CHADEMA) kwa kutaka kufanya mkutano wa hadhara bila ya kuwa na kibali.

Mollel alikamatwa jana, saa nane mchana, wakati akitaka kufanya mkutano katika kijiji cha Miti Mirefu, jimboni humo, ambapo inahisiwa kuwa ni mwendelezo wa mikutano wanayotaka kufanya viongozi wa upinzani.

Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa mbunge huyo zilisema kuwa, baada ya kukamatwa, alifikishwa katika kituo cha Polisi Sanya Juu kwa lengo la kuhojiwa, lakini baadaye aliondolewa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi mkoa wa Kilimanjaro.

Wakati mbunge huyo akiwa njiani kupelekwa kituo hicho,
aliwapigia simu waandishi wa habari kwa lengo la kuwaeleza kuwa amekamatwa na jeshi hilo.

“Ni kweli nimekamatwa na polisi na hivi sasa napelekwa Moshi kwa ajili ya kuhojiwa, baada ya hapo nitawatafuta waandishi wa habari ili kuwaelezea nini kilichotokea,” alisema Mollel.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema  mbunge huyo alikuwa akitaka kufanya mkutano kinyume na sheria wakati imezuiwa kwa sababu za kiusalama.

Kamanda Mutafungwa alisema baada ya kuona maandalizi ya mkutano huo, ndipo jeshi hilo lilipoamua kumwita na kumhoji na kumtaka asiendelee na mkutano huo.

No comments:

Post a Comment