Wednesday 8 June 2016

POLISI WAMUHOJI ZITTO KWA SAA TATU

JESHI la Polisi limemhoji Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT), Kabwe Zitto kwa takribani saa tatu, kufuatia kauli alizozitoa Jumapili iliyopita, kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya Zakhiem, Mbagala, Dar es Salaam.

Mahojiano hayo yalifanyika jana, Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kuanzia saa 3.30 asubuhi hadi saa 6.15 mchana, ambapo Kamishna wa kanda hiyo, Simon Sirro, alisema ni kawaida kwa jeshi hilo kufanya hivyo kwa yeyote, inapoona kuna umuhimu ya kufanya hivyo.

“Hakuna aliye juu ya sheria, akiwemo Zitto, hivyo kama kulikuwa na sababu ya kumhoji, amehojiwa, nitapata taarifa baadaye juu ya mahojiano hayo, ndipo nitakuwa na mambo zaidi ya kuzungumza,” alisema Kamishna Sirro.

Akizungumza baada ya mahojiano hayo, Zitto alisema ameshangazwa na kitendo cha polisi kumhoji kwa kuwa haoni suala la msingi, badala yake alidai hivyo ni viashiria vya kuminywa kwa demokrasia nchini.

Alisema amehojiwa karibu kila kitu alichozungumza katika mkutano huo, jambo linalodhihirisha demokrasia inatoweka na kwamba, hali hiyo imemsikitisha.

Zitto pia alisema anasikitika kuona polisi ikisitisha mikutano ya kisiasa kote nchini na kusema kuwa si sahihi kwa jeshi hilo kufanya hivyo, kwa kuwa jukumu lake si kuzuia, isipokuwa kulinda usalama na utulivu.

Alisema wanasheria wake wanasubiri uchunguzi ukamilike na iwapo jambo hilo litapelekwa mahakamani au la, nao watajua nini cha kufanya na kwamba, kamwe hawatakubali kuminywa kwa demokrasia kwa kuwa wameipigania kwa muda mrefu.

Juni 5, mwaka huu, Zitto na viongozi wengine waandamizi wa Chama cha ACT-Wazalendo, walifanya mkutano wa hadhara katika viwanja hivyo, vilivyoko Mbagala na kuzungumza mambo mbalimbali, yakiwemo yaliyolenga kuishambulia serikali kutokana na uamuzi mbalimbali inaouchukuwa, ikiwemo uamuzi wa haraka kwenye baadhi ya mambo ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment